Mara Paa! Bale ndani Man Utd, Neymar anatua Real

Muktasari:

  • Los Blancos wameripotiwa kuweka pesa nyingi sana kwenye dau la kumuuza Bale ili kupunguza machungu yao ya kutumia pesa nyingi wakati watakapokwenda kupeleka ofa huko Ufaransa kumnyakua Mbrazili Neymar.

Madrid, Hispania. Real Madrid wanawasikilizia Manchester United na mpango wao wa kumsajili Gareth Bale kwani wao wanataka fedha itakayopatikana kwenye mauzo hayo wazichangechange kumbeba Neymar kutoka Paris Saint-Germain.


Los Blancos wameripotiwa kuweka pesa nyingi sana kwenye dau la kumuuza Bale ili kupunguza machungu yao ya kutumia pesa nyingi wakati watakapokwenda kupeleka ofa huko Ufaransa kumnyakua Mbrazili Neymar.


Baada ya kubeba mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika kipindi chake cha miaka mitano huko Madrid, Bale amesema sasa anataka kucheza kila wiki na hilo atalifanya hata kwa timu ya nje ya jiji hilo la Hispania.


Kauli hiyo ina maana Bale anajiandaa kuhama huku Man United wakitajwa ndio wanaonekana kutoa macho kwenye kuwinda huduma ya staa huyo wa kimataifa wa Wales.


Real Madrid inamtazama Bale kuwa na thamani ya Pauni 195 milioni, licha ya mkataba wa mchezaji huyo kuwekewa kipengele cha Pauni 1 bilioni kwa timu itakayotaka kumnunua.

Madrid wanataka pesa kurahisha mpango wao wa Neymar, hivyo wanawasikilizia Man United pumzi yao.