Manara amkingia kifua kocha Minziro

ARUSHA. MSEMAJI wa timu ya Simba SC, Haji Manara ameonekana akimpigia debe Kocha Mkuu wa timu ya Arusha United, Fredy Felix ‘Minziro’ asitimuliwe na kumwaga sifa kuwa ni moja ya makocha bora wazawa kwenye ligi za Tanzania.

Manara alimwomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye ndie Mlezi wa timu hiyo kuwa anauhakika na anamwamini Minziro ataonesha soka la tofauti mkoani hapa na atawafikisha sehemu sahihi wanapotaka.

“Naomba msije mkamsahau atakapoipandisha timu Ligi kuu maana tumeona alipotoka kila jema alilolifanya limeonekana bure, lakini nakuamini na ninakuomba hilo lisije likatokea kwako utakuwa hujatenda haki kwani utaumiza moyo wake na wangu pia kama atapandisha timu halafu akaondolewa,” alisema Manara.

Aliongeza kuwa Minziro ataipandisha timu hiyo Ligi kuu kama watampa ushirikiano wa kutosha kwani analijua vyema soka la Tanzania ndani na nje ndio maana anapata mafanikio kila anapokwenda na kuipandisha Singida United na KMC msimu uliopita.

Manara alikuwa Mkoani hapa na timu ya Simba walipokuja kucheza mchezo wa Kirafiki dhidi ya Arusha United na kuibuka na ushindi wa bao 2-1 yote yakifungwa na Emmanuel Okwi dakika 7 na 29 huku lile la wenyeji likifungwa na Ally Kabunda dakika 17.

 

Msemaji huyo aliapa kujihudhuru nafasi yake mapema kama timu yake ingefungwa kwenye mchezo kwa madai haoni sababu yeye kuendelea kuongoza na kufungwa na timu hiyo.