Mambo,manne,yaibeba,Z'bar,leo

Muktasari:

  • Kenya imetwaa ubingwa wa Chalenji mara sita wakati Zanzibar ikitwaa ubingwa huo mara moja.

Ubora wa kikosi, presha ya wenyeji, nidhamu ya mchezo, ari ya wachezaji pamoja na mbinu za kocha Hemed Morocco, ni mambo manne yanayoipa Zanzibar nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya Chalenji leowatakapoumana na Kenya kwenye mchezo wa fainali kwenye Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos huko Kenya.

Zanzibar inaingia uwanjani katika mchezo huo ikiwa ni moja ya timu zenye vikosi bora zaidi katika mashindano hayo yanayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kutokana na namna kikosi chake kinavyoweza kubadilika kulingana na ubora na mbinu za timu pinzani sambamba na mwitikio wao chanya pindi timu pinzani wanapotanguliwa kufungwa, kufunga au wapinzani wanaposawazisha bao.

Presha ya wenyeji Kenya ambao watacheza mbele ya maelfu ya mashabiki wao, ni faida nyingine kwa Zanzibar ambayo itacheza bila presha kubwa kutokana na kutokuwa na cha kupoteza lakini pia kingine ni nidhamu ya hali ya juu ambayo wachezaji wa Zanzibar wamekuwa nayo katika kulinda lango, kushambulia na kumiliki mpira.

Jambo lingine ambalo litakuwa na faida kubwa kwa Zanzibar leo ni ari na hamasa ya wachezaji wake ambao wanaitolea macho zawadi ya Dola 30,000 (Shilingi 67 Milioni) wakiamini itawasaidia kujiliwaza kutokana na hali ngumu ya ukata ambayo wamepitia kuanzia wakati wa maandalizi hadi sasa walipoingia hatua hiyo ya fainali.

Kingine ambacho Zanzibar wanajivunia ni mbinu za kocha wao Morocco ambaye amekuwa na uwezo wa hali ya juu wa kuisoma mchezo na timu pinzani na pia kutumia udhaifu aliouona na kuufanyia kazi kwa haraka jambo ambalo limekuwa likiibeba timu hiyo.

Kocha Hemed Morocco ana furaha leo kwa kurejea kwa beki wake wa kushoto Haji Mwinyi ambaye alikosa mchezo uliopita wa nusu fainali dhidi ya Uganda kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.

Morocco aliliambia gazeti hili kuwa wanatambua mchezo huo utakuwa mgumu sana kwani wanawakabili wenyeji ambao hatua ya makundi walitoka nao suluhu lakini  lazima wahakikishe wanatimiza malengo yao ya kutwaa ubingwa.

"Itakuwa mechi ngumu kwa sababu kwanza ni mchezo wa fainali  kila mmoja anataka heshima,lakini pia tunacheza na wenyeji wako kwao hivyo watakuwa na sapoti kubwa ya mashabiki wao.

"Sina hofu kwani nina kikosi imara na nimewaambia wachezaji wangu wanapasa kuongeza nguvu ya kupambana ili kuweza kutwaa ubingwa na kuitoa kimasomaso Zanzibar na Tanzania kwa ujumla"alisema Morocco.

Tayari Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewapongeza kwa mafanikio hayo na kuahidi mapokezi makubwa yanaandaliwa kwa ajili yao.

 “Natoa pongezi za dhati kwa wachezaji wote wa “Zanzibar Heroes” pamoja na viongozi wao kwa mafanikio makubwa waliyotuletea hadi kufikia hatua ya fainali ya mashindano hayo”,alisema Dk. Shein.

Dk. Shein zilieleza maandalizi ya kuwapokea na kuwarudisha nyumbani yameshaanza kupitia uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo.

Zanzibar imetwaa ubingwa wa mashindano hayo mara moja tu ilikuwa mwaka 1995 walipoifunga Uganda bao 1-0, ambayo safari hii waliitoa kwenye mchezo wa nusu fainali kwa ushindi wa mabao 2-1.