Mamba matano ujio wa Juuko Simba

Muktasari:

Kutokana na ubora na kiwango chake, wengi wanajiuliza anaweza kuingia vipi kwenye kikosi cha kwanza ukizingatia kuwa tayari safu ya ulinzi ya timu hiyo ina mabeki wawili wa kiwango cha juu, wenye uzoefu na walioelewana ambao ni Paschal Wawa na Erasto Nyoni.

Dar es Salaam. BAADA ya kujiweka nje ya kikosi cha Simba kwa zaidi ya miezi mitano, hatimaye beki raia wa Uganda, Juuko Murshid amerejea nchini wiki hii kujiunga na klabu yake.
Juuko ni miongoni mwa mabeki bora wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutokana na uzoefu na uwezo wa hali ya juu alionao na ni wazi kwamba kurejea kwake kutaongeza uimara wa kikosi cha Simba hasa kwenye safu ya ulinzi.
Amekuwa tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya Taifa ya Uganda kwa zaidi ya miaka minne jambo lililomfanya apate fursa ya kupambana na kundi kubwa la washambuliaji tishio duniani ambao alifanikiwa kuwadhibiti kama Mohammed Salah, Andrew Ayew, Jordan Ayew, Emmanuel Adebayor na Jonathan Pitroipa.
Kutokana na ubora na kiwango chake, wengi wanajiuliza anaweza kuingia vipi kwenye kikosi cha kwanza ukizingatia kuwa tayari safu ya ulinzi ya timu hiyo ina mabeki wawili wa kiwango cha juu, wenye uzoefu na walioelewana ambao ni Paschal Wawa na Erasto Nyoni.
Ifuatayo ni tathmini ya mambo matano ambayo benchi la ufundi la Simba linaweza kuyafanya ili Juuko aingie kikosi cha kwanza.

1.KUBADILI  MFUMO
Chini ya Kocha Patrick Aussems, Simba imekuwa ikitumia mfumo wa 4-4-2 ambapo imekuwa ikiwatumia Nyoni na Wawa kama mabeki wa kati.
Kutokana na ujio wa Juuko na ubora wa Wawa na Nyoni, Aussems anaweza kutamani kuwaanzisha kwa pamoja mabeki hao wote wa kati ili kutengeneza ukuta imara zaidi kupitia mifumo ya 3-4-3 au 3-5-2 na hili linaonekana halitoisumbua Simba kwani tayari walishawahi kucheza kwa mifumo hiyo chini walipokuwa na maocha Pierre Lechantre na Masoud Djuma.

2. KAPOMBE KUCHEZA WINGA
Simba inaweza kubaki kwenye mfumo wake ilioanza nao msimu wa 4-4-2 lakini ikaamua kufanya mabadiliko ya nafasi za wachezaji ndani ya uwanja kwa kumsogeza beki wa kulia, Shomary Kapombe kucheza kama winga na kisha Nyoni kupelekwa kuziba nafasi yake huku Juuko akipangwa kati kucheza na Wawa.

3.NYONI  KUMPUMZISHA KOTEI/MKUDE
Erasto Nyoni ana uwezo wa hali ya juu kucheza nafasi tofauti ndani ya uwanja hivyo kutokana na ujio wa Juuko, benchi la ufundi la Simba linaweza kumrudisha benchi kiungo mmojawapo kati ya Jonas Mkude au James Kotei na nafasi yao kupangwa nyota huyo wa zamani wa Azam FC.
Kitendo cha Nyoni kusogezwa kwenye kiungo kutampa nafasi Juuko kuchezeshwa na Wawa sambamba kama mabeki wa kati.

4.WAWA  KUKALIA  BENCHI
Paschal Wawa ni beki anayetumia akili, nguvu na hesabu za hali ya juu pindi anapokabiliana na washambuliaji wa timu pinzani lakini umri wake unaonekana kusogea na kuna nyakati hushindwa kuwadhibiti wachezaji wenye kasi.
Kutokana na hilo, benchi la ufundi la Simba linaweza kuamua kumpumzisha pindi wanapokutana na wapinzani wenye washambuliaji walio na kasi na kuwapanga sambamba Nyoni na Juuko.

5.KWASI KUGOMBEA NAMBA NA NYONI
Erasto Nyoni anaweza kuwa muhanga wa kumpisha Juuko lakini asiumizwe sana na mabadiliko hayo kwani bado jeuri na uwezo wa kucheza nafasi nyingi utaendelea kumbeba na huenda akarudishwa kwenye nafasi aliyoanza nayo pindi aliposajiliwa na Simba ya beki wa kushoto.
Ikiwa hilo litatokea, Asante Kwasi anayecheza nafasi hiyo kwa sasa atalazimika kufanya kazi ya ziada ili asipoteze namba mbele ya mkongwe huyo na kujikuta akikaa benchi ama atalazimika kucheza kama winga wa kushoto.

AUSSEMS  AMESHIKILIA  RUNGU
Hata hivyo pamoja na uwezekano wa kutokea mambo hayo matano hapo juu, bado uamuzi wa mwisho wa Juuko kucheza au kutocheza utatokana na utashi na uamuzi wa kocha Patrick Aussems na benchi lake la ufundi.
Ikiwa beki huyo atafanikiwa kulishawishi, basi litampa nafasi kwenye kikosi cha kwanza lakini vinginevyo anaweza kujikuta akisotea benchi.