Malale anaanza upya Ndanda FC

NDANDA FC kwa misimu mitatu mfululizo imekuwa ikinusurika kushuka daraja, lakini safari hii Kocha Mkuu wake, Malale Hamsini ameweka wazi mikakati yake ya kuhakikisha timu inafanya vizuri msimu mpya wa Ligi Kuu.

Malale alisema amepata jeuri ya kuamini Ndanda ya sasa imezaliwa upya kutokana na aina ya wachezaji iliyowasajili baada ya asilimia kubwa ya kikosi chake cha kwanza cha msimu uliopita kutimka klabu nyingine na kusuka upya timu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Malale alidai licha ya tatizo la ukata unaoikabili timu hiyo na kuchelewesha kuanza mazoezi bado anaamini ana muda wa kuwajenga wachezaji wake kuelekea msimu mpya.

Kocha huyo alikiri timu yake inapitia kipindi kigumu kwa vile hadi jana walikuwa hawajaanza maandalizi kutokana na ukata na kuweka wazi atakuwa na kazi ngumu kuhakikisha anaonyesha ushindani kwenye ligi inayotarajia kuanza Agosti 22. Hata hivyo, anaamini wakizoeana Ndanda itakuwa moto kwa vile wachezaji wanaonekana kuwa na morali.