Majimaji mjipange kwa Mwadui

KAMA Majimaji inauchukulia poa mchezo wao dhidi ya Mwadui katika mfululizo wa Ligi Kuu Bara itakayoendelea wiki ijayo, itakula kwao, kwani wenyeji wao wamepania kuwafanyizia watakapokutana Aprili 8.
Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu alisema mechi yao dhidi ya Majimaji, wapinzani wao wasitegemee mteremko kabisa kwani wamepania kutoka na ushindi.
Bizimungu alisema wanahitaji ushindi ili kurudisha hali ya kujiamini katika kikosi chake, baada ya kupoteza michezo ya awali na pia kutaka kuondoka eneo la mkiani.
"Tumebakiza michezo mitano nyumbani, tunatakiwa tushinde yote ili tuwe katika sehemu nzuri hivyo hao wanaoluja huku wajipange kabisa," alisema Bizimungu.
Akizungumzia programu yake aliyokuwa akiiendesha kufanya mazoezi mara tatu kwa siku, alisema programu hiyo inaendelea vizuri baada ya wachezaji kuipokea vizuri.
Majimaji ndio inayoburuza mkia ikiwa na alama 16 pekee baada ya mechi 22 na kujiweka katika janga la kushuka daraja kama haitajipanga vema kwa mechi zake za lala salama.