MZUKA: Wakongwe wanogesha kwa kushusha nondo

ILIANZA kama masihara, lakini sasa ni utamaduni wao.

Ukisikia Agosti 8 najua kumbukumbu zako zinakupeleka kwenye Sikukuu ya Wakulima. Hata hivyo, hii sio tu sikukuu, ni siku maalumu ya Wanasimba. Wao wameipa jina la SIMBA DAY.

Simba iliyoasisiwa Agosti 8, 1936, leo inatimiza miaka 82 na kama kawa kila mwaka hufanya utambulisho wa wachezaji wapya na jezi ikiwa ni pamoja na kuialika timu mojawapo kubwa Afrika kunogesha sherehe hizo za aina yake na mwaka huu wakiwaalika Asante Kotoko ya Ghana kuvaana nao kwenye Uwanja wa Taifa zitakapofanyika sherehe hizo.

Sherehe hizo huenda sambamba na kufanya mambo ya kijamii na kutuza wadau wao muhimu wakiwemo wakongwe.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na baadhi ya wachezaji wao wa zamani ambao wanamitazamo yao tofauti kuhusu siku hii maalumu.

ULIMBOKA MWAKINGWE

Winga wa zamani wa timu hiyo, ametamka bila kificho haoni manufaa ya sherehe hizo kwa kuwa hazizingatii malengo sahihi, badala yake imegeuka kama dili kwa kupiga pesa kwa wanaotaka kujinufaisha kupitia hilo.

“Malengo ya sherehe hizo ilikuwa ni kufanya vitu tofauti vyenye ubunifu kwa klabu yetu, lakini kwa sasa unaona wanaendesha mambo kisiasa, ninachoshauri wafanye vitu vya umakini vitakavyowafurahisha wanachama wao. Utoaji wa tuzo kwa wachezaji wa zamani ni kitu kizuri, lakini wanatakiwa waongeze idadi kwani wapo wengi waliofanya vitu vikubwa kwa nyakati tofauti,” anasema

MRAGE KABANGE

Winga wa zamani wa timu hiyo. Yeye anasema Simba Day inatendewa haki kwani tangu ianzishwe ina mwendelezo, huku akishauri viongozi waboreshe upande wa mechi za kirafiki wanazocheza siku hiyo.

“Inachosha kila wakati mara wamechukua timu kutoka Uganda, Kenya wabadilishe awamu hii walete angalau TP Mazembe hata kama tutafungwa, lakini kuna vitu vya kujifunza katika klabu hiyo yenye mafanikio kwa Afrika. Kwa upande mwingine inatoa nafasi kwa viongozi kubadilishana mawazo na wanachama wao, inawatambulisha nyota wao wa zamani ambao walifanya mambo mazito ndani ya timu hiyo,” anasema.

ZAMOYONI MOGELLA

Ni kati ya wachezaji wanaokumbukwa ndani ya klabu hiyo kwa kufanya mambo makubwa enzi hizo. Anashauri Simba Day iwe ya kuongeza kipato kwa klabu hiyo, kwa maana ya viongozi kutafuta watu wa masoko ambao wataleta wadhamini siku hiyo.

“Naona Simba Day ni kitu kizuri, lakini wasiishie kukaa vikundi vya watu wachache ndio wafanye uamuzi wa kila kitu kwa siku hiyo, ifike hatua wawe na ubunifu, kama kutafuta watu wa masoko ambao watatengeneza upatikanaji wa pesa kwa siku yenyewe isiwe ya ovyo ovyo.

“Simba imepata mdhamini makini ila nina shaka na wale ambao wanamzunguka pembeni, inakokwenda itakuwa klabu yenye mfano kwa Afrika, kutokana na hilo lazima wafanye vitu kisomi, mfano katika siku hiyo kuonekane vitu vipya tofauti na zamani,” alisema.

FRANK KASANGA ‘BWALYA’

Beki wa zamani wa kati wa timu hiyo, anasema uwepo wa siku hiyo unawakutanisha Wanasimba na kukumbuka walikotoka, walipo na wanakoelekea, hivyo alisisitiza ni jambo la kujivunia.

“Kikubwa wanachotakiwa kukifanya viongozi ni kutoa nafasi kwa wachezaji wote waliowahi kuitumikia Simba, kwa upana wake na sio kuangalia waliopo Dar es Salaam pekee ambako ndio makao makuu ya timu hiyo.

“Wakizingatia hilo Simba itakuwa mfano kwa klabu za ndani na nje, kwani watatoa michango yao ya nini kifanyike ili wachezaji wawe bora na kucheza kwa viwango vya kimataifa, iwe siku yenye kufanya vitu vya kihistoria ambavyo vitawafunza masta wa sasa,” alisema.