Simba yamtuliza Mo Ibrahim

Muktasari:

Kiungo ameshindwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Simba msimu huu.

Dar es Salaam. Mashabiki wa Simba wana presha na hofu ya kumpoteza kiungo wao mshambuliaji, Mohammed Ibrahim 'MO' ambaye Yanga wanamnyatia kimyakimya kama wanafukuza mwizi gizani.

Lakini mpaka jana Jumatatu, Simba ambayo ina mkataba na mchezaji huyo ilimtuliza akili na kumhakikishia kwamba maisha yatakuwa safi tu, aendelee kujituma na Meneja wake amewaambia watulize mzuka kijana atabaki Msimbazi.

Meneja wa kiungo huyo ambaye Simba ilimsajili kutokea Mtibwa wakati wa dirisha kubwa la usajili mwaka 2016, Jamal Kisongo alilithibitishia gazeti kuhusu ofa mbalimbali ambazo amezipokea kutoka kwa timu zinazomhitaji kiungo huyo ikiwemo ya Yanga, lakini amefichua kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa mchezaji kubakia Simba labda tu wenyewe wabadilike dakika za mwishoni.

"Kwanza ifahamike wazi kwamba hadi sasa, Mohammed Ibrahim ni mchezaji halali wa Simba ambaye bado mkataba wake haujamalizika. Kuhusu ofa ni kweli tumepokea ofa nyingi ikiwemo na Yanga na hii inaashiria kwamba yeye ni mchezaji mzuri kwani kitendo cha kuwaniwa na timu nyingi kinaashiria wazi kwamba kiwango na ubora wake ni wa hali ya juu.

"Tumefanya mazungumzo na uongozi wa Simba mara kadhaa na kiukweli wameonyesha nia ya kumbakiza na tayari tumeshawapa mchanganuo wetu wa vitu tunavyovihitaji ambao wameniambia wameshaanza kuufanyia kazi lakini pia leo (jana), mimi binafsi nitakutana na mchezaji wangu.

"Lengo ni kujadiliana juu ya kile ambacho Simba wanakihitaji kwetu na Mungu akipenda tutakamilisha hili suala mapema," alisema Kisongo.

Hata hivyo kama dili hilo la Ibrahim kubakia Simba litafanikiwa, kipa Aishi Manula huenda akawa ni mwenye kicheko zaidi kuliko mtu mwingine yeyote kutokana na nyota ya bahati ya kiungo huyo.

Kismati ambacho Mohammed Ibrahim amekuwa nacho kwa Simba msimu huu ni kile cha nyavu za timu hiyo kutotikisika katika mechi zote za Ligi Kuu ambazo kiungo huyo amekuwepo katika orodha ya wachezaji 18 wa wanaopaswa kutumika katika mchezo wa ligi.

Nyavu za Simba zimetikisika katika mechi nne za Ligi Kuu hadi sasa dhidi ya Mtibwa Sugar, Mbao, Yanga na Stand United lakini zote hizo kiungo Mohammed Ibrahim hakuwepo kwenye kikosi cha kwanza wala katika orodha ya wachezaji saba wa benchi.

Cha ajabu, timu hiyo haikuruhusu bao katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting, Azam FC, Mbeya City na Prisons ambazo zote kiungo huyo fundi alikuwemo kwenye orodha ya wachezaji 18 wanaotumika kwenye mechi husika.