Lukaku ajitetea Man United

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo amekuwa na rekodi ya kushindwa kufunga kila anapocheza na timu kubwa

Mshambuliaji wa a Manchester United, Romelu Lukaku amesema anafahamu watu wanavyosema juu yake kwamba hafungi kwenye mechi kubwa, mbona walikaa kimya alipowafunga Real Madrid.

Mshambuliaji huyo amefunga mabao 11 katika mechi 11 alizochezea Man United msimu huu, amekosolewa baada ya kushindwa kuwafunga Liverpool kwenye Ligi Kuu England Jumamosi iliyopita, lakini akawajibu wanaomfuatilia kwa kuwaaambia nani wakali kati ya Liverpool na Real Madrid?

Lukaku alisema kwamba anafahamu kwa sasa watu watakuwa wakimfuatilia sana baada ya kutua Man United, lakini hata alipokuwa Everton mechi nyingi tu alikuwa hafungi. Lukaku aliifunga Real Madrid katika mechi ya kipigo cha mabao 2-1 kwenye mchezo wa Uefa Super Cup.

"Nadhani kama ni presha basi ilikuwa kwenye mechi ya Uefa Super Cup dhidi ya Real Madrid, kwa sababu kila mtu alikuwa akitazama mechi ile. Watu waliniangalia sana kwenye mechi ile, na nadhani kimetokea kilichotokea. Watu huwa hawachoki kusema, lakini rekodi zangu kwenye Ligi Kuu England msimu huu zipo vizuri," alisema Lukaku.

Mshambuliaji huyo kesho Jumatano atashuka uwanjani kuiongoza timu yake Man United kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo wababe hao wanaonolewa na kocha Jose Mourinho watakuwa ugenini huko Ureno kumenyana na Benfica.

Wakati huo huo, staa wa zamani wa Liverpool, Jamie Redknapp amewashangaa watu wanaomsema Mourinho kwamba amepaki basi dhidi ya Liverpool na kumwaacha kocha Jurgen Klopp, ambaye ndiye hasa aliyetaka sare katika mechi hiyo. Redknapp alisema anamwelewa Mourinho mpango wake, kwamba alikwenda kwenye mechi hiyo asifungwe kitu ambacho kilifanikiwa, lakini Klopp katika kipindi ambacho alipaswa kutafuta ushindi, aliwatoa wachezaji wake muhimu Mohamed Salah na Philippe Coutinho na kuhoji sasa hapo aliyetaka sare ni nani?

"Wakati zimebaki dakika 10, Man United walionekana kuchoka, lakini Klopp akwatoa Mo Salah na Philippe Coutinho, wachezaji wawili waliokuwa tishio kweli kweli siku ile. Sasa hapo utamlaumu vipi Mourinho, Klopp ndiye aliyetaka sare kwenye mechi ile," alisema Redknapp.