Luhende achimba mkwara Kagera Sugar

Muktasari:

  • Mkongwe huyo aliyewahi kung’ara na Yanga amejiunga na Kagera Sugar kwa kandarasi ya mwaka mmoja akitokea Mwadui.

Mwanza. Baada ya kujiunga na Kagera Sugar, beki wa kushoto David Luhende amesema licha ya uwezo na uzoefu alionao katika soka ataingia kwa umakini kuhakikisha hakosi namba kwenye kikosi cha kwanza.
Mkongwe huyo aliyewahi kung’ara na Yanga amejiunga na Kagera Sugar kwa kandarasi ya mwaka mmoja akitokea Mwadui.
Luhende alisema hana wasiwasi na uwezo wake katika soka, lakini ataingia kwa tahadhari kwa kuonyesha uwezo ili kulishawishi benchi la ufundi ili kumpanga katika kikosi cha kwanza kila mchezo.
Alisema kwa sasa anaendelea na mazoezi yake binafsi akisubiri kuitwa kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu na kwamba anajua kila kocha huwa na uamuzi yake.
Beki huyo aliongeza kuwa anaamini ushindani utakuwapo kutokana na wachezaji waliopo Kagera Sugar kuwa bora, lakini yeye anahitaji kuonyesha uwezo na utofauti wake katika kuisaidia timu.
Alisema kuwa anaamini chini ya Kocha Mecky Mexime kiwango chake kitaongezeka zaidi na kwamba atakuwa makini kusikiliza maelekezo kwa manufaa yake katika kazi hiyo ya soka.
“Lazima ushindani utakuwapo kwa sababu kila mmoja anataka acheze mpira,lakini kikubwa ni kuisaidia timu kuhakikisha inafanya vizuri naamini nitafanikiwa,”alisema beki huyo.