Mabeki Liverpool walaumiana

Muktasari:

  • Liverpool msimu imekuwa na safu mbovu ya ulinzi iliyoruhusu mabao mengi

Mabeki wa Liverpool nusura wazichape kavukavu uwanjani katika mchezo waliobugizwa mabao 4-1 na Tottenaham Hotspurs.

Liverpool juzi usiku iliogelea mvua ya mabao katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa Uwanja wa Wembleya ambao Spurs ilikuwa mwenyeji.

Nahodha wa timu hiyo Jordan Henderson alikaribia kumvaa maungoni beki Joel Matip baada ya kuruhusu bao la kizembe.

Akionekana kuchukizwa na safu ya ulinzi, Henderson aliwabwatukia mabeki Matip na Dejan Lovren akidai walikuwa uchochoro.

Harry Kane aliyefunga mabao mawili katika mchezo huo, alikuwa mwiba kwa Lovren, aliyetolewa dakika ya 31 baada ya kucheza chini ya kiwango.

Kocha wa timu hiyo Jurgen Klopp, alisema haamini kilichotokea katika mchezo huo na alishangazwa na kiwango cha chini kutoka kwa mabeki wake.

Mjerumani huyo alidokeza Spurs ilipata mabao 'laini' na endapo angekuwa uwanjani enzi zake angezuia mvua hiyo.

Liverpool imefungwa jumla ya mabao 16 katika mechi tisa za Ligi Kuu England msimu huu. Pia imechapwa mabao 12 katika mechi tatu walipotoka sare ya mabao 3-3 na Watford, ilinyukwa 5-0 na Manchester City kabla ya kulala 4-1 dhidi ya Spurs.