Kwa utatu huu, mwageni zege

Muktasari:

  • Hata hivyo, wapo washambuliaji wengine, kazi yao kubwa ni kuhakikisha timu inapata matokeo. Wao kwa wakati wote wakipangwa pale mbele hawataki kujua ni nani atafunga, zaidi wanachotaka ni matokeo mazuri.

INAPOKUJA ishu ya ufungaji mabao kwa timu yoyote, wanaotupiwa macho kwa ukaribu zaidi ni washambuliaji. Hawa ndio wenye kazi yao, achana na wale mabeki au viungo wanaopanda na kufunga na kuwapita kwa mabao hata washambuliaji. Sio kazi yao sana, ila wakipata nafasi hiyo wanawasaidia.

Hata hivyo, wapo washambuliaji wengine, kazi yao kubwa ni kuhakikisha timu inapata matokeo. Wao kwa wakati wote wakipangwa pale mbele hawataki kujua ni nani atafunga, zaidi wanachotaka ni matokeo mazuri.

Unakumbuka ule utatu wa mastraika wa Barcelona, Lionel Messi, Luiz Suares na Neymar (MSN) ama ule wa Real Madrid wa Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na Karim Benzema? Upo utatu wa aina hiyo kila mahali na unaambiwa kama akikosekana mmoja, lazima uone tofauti.

Ligi Kuu Bara ikiwa imeingia raundi ya tatu, baadhi ya timu zikiwa zimeshaonyesha ni hatari hasa eneo la ushambuliaji.

Hata hivyo, huku ligi ikiwa inaendelea, Mwanaspoti limemulika utatu wa baadhi ya washambuliaji ndani ya vikosi vyao na kuona kama watasimama pamoja pale mbele, ni wazi timu pinzani lazima zijipange kwani utatu huo utawasha moto.

SIMBA

- Kagere, Okwi, Kichuya (KOK)

Pale Simba kwa sasa kila mtu anakenua. Viongozi na mashabiki wake wana furaha sana. Achana na ishu ya timu kupewa mmiliki Mohamed Dewji. Achana na mabilioni yao ya usajili, furaha ya Simba inazidi kwa sababu ya safu yao ya ushambuliaji. Kwa usajili walioufanya, Simba wameweza kutengeneza safu bora ya ushambuliaji na kama wataitumia vyema, mwishoni mwa msimu lazima watetee taji lao.

Japo Simba inaweza kuongoza kwa kuwa na washambuliaji wengi hatari wakiwamo chipukizi kama Adam Salamba, Marcel Kaheza ama Mohammed Rashidi, lakini kuna majembe matatu matata.

Pale mbele kuna watu wana kiu ya mabao, Meddie Kagere aliyetupia mabao matatu kwa sasa katika mechi tatu ya Ligi Kuu, Shiza Kichuya na Emmanuel Okwi ni hatari. Hapo John Bocco hujamtaja kabisa. Japo Kagere na Okwi hawajakutana kwa vile Mganda huyo ni majeruhi, lakini fikiria kwa utatu huu, we ukipenda waite kwa kifupi BOK, wakicheze pamoja pale mbele unadhani nini kitatokea.

Hicho ndicho Simba kwa sasa inajivunia. Washindwe wenyewe tu.

YANGA

-Ngassa, Ajibu, Makambo (MAN)

Kwa sasa pale Yanga anayetazamwa zaidi ni Heritier Makambo. Amekuwa mfalme kwa sababu ya mavitu yake yanayowapa raha Wanajangwani. Hadi sasa tayari ameshatupia mabao mawili katika michezo miwili aliyocheza.

Yanga pia ilimsajili Mrisho Ngassa kuongeza nguvu katika kikosi chake japokuwa bado hajaziona nyavu hadi sasa. Pia, kuna Ibrahim Ajibu ambaye amekuwa hapewi nafasi na Kocha Mkongomani, Mwinyi Zahera ingawa ana kiwango chake kizuri cha msimu uliopita kulizinyanyasa baadhi ya timu Ligi Kuu.

Hata hivyo, fikiria kwa kiwango cha sasa cha Ajibu, ubora wa Makambo anayetazamwa kama mwokozi pale Jangwani pamoja na Ngasa ambaye amerudi na moto wake, kama atapenda waite ‘MAN’, ni wazi wapinzani lazima wajipange na vile ligi ndio kwanza mbichi, wana nafasi kubwa ya kuibeba Yanga na kuurudisha utawala wao wa Ligi Kuu na kimataifa.

AZAM FC

- Kutinyu, Lyanga, Mahundi (KNL)

Msimu ndio kwanza umeanza lakini moto wa safu ya ushambuliaji ya Azam FC umeonekana kuwaka kwa kasi zaidi.

Azam FC inaongoza kwa ufungaji huku ikifunga idadi kubwa ya mabao katika mechi michezo miwili tu, mabao matano.

Hata hivyo, kwa mabao hayo, utatu unaouona hapo juu kama ukipenda uite KLM, yaani Tafadzwa Kutinyu, Danny Lyanga na Joseph Mahundi.

Safu hiyo inaweza kuwa kali zaidi kama straika Donald Ngoma atarudi kuanza kwenyye kikosi hicho. Nani hajui makali ya Ngoma uwanjani?

Kutinyu tayari ana mabao mawili hadi sasa akiitungua Ndanda FC katika ushindi wa mabao 3-0, huku jingine kiliwekwa kimiani na Mahundi aliyefunga pia dhidi ya Mbeya City.

Stori ya Danny Lyanga haitafautiani sana na Mahundi kwani ameshatupia bao moja dhidi ya Mbeya City katika ushindi wa mabao 2-0. Hapa anayesubiriwa kwa sasa ni Ngoma ambaye alijiunga na Azam akitokea Yanga. Bado hajawa na msimu mzuri lakini ikiwa ndio kwanza ligi mbichi, ni wazi akiungana na wenzake hadi ligi ikimalizika, watakuwa wana hazina ya mabao ya kutosha na wakikaza tu watatoboa hadi ubingwa. Tusubiri tuone mchezo unaofuata wa Azam kama mwalimu atampa nafasi kutokana na kuanza mazoezi na wenzake.

MBAO FC

- Said, Athanas, Mujwahuki (SAM)

Pacha ya washambuliaji hao tayari imeshaonyesha maajabu katika ligi inayoendelea kutokana na kuwasumbua zaidi mabeki katika michezo miwili tu na kuvuna pointi tatu. Yaani kuna Said Khamis, Pastory Athanas na Evaligestus Mujwahuki.

Mujwahuki alianza kuonyesha ubora wake katika mchezo dhidi ya Alliance naye ndiye aliyefunga bao la ushindi dakika ya 80 ambalo lilidumu hadi dakika 90 za mchezo Said Khamis alimjibu kwa kufunga bao la penalti katika mchezo dhidi ya Stand United.

Pastory Athanas naye hakutaka kubakinyuma katika pacha hiyo iliyoibeba timu yao kushinda mfululizo katika michezo miwili iliyocheza baada ya kufunga bao moja na la ushindi katika mchezo wao dhidi ya Stand United iliyoibuka kwa ushindi wa bao 2-1. Hapa inatuonyesha hii SAM itakuwa moto zaidi hadi ligi itakapokwisha na sio siri wakaipa matokeo mengi mazuri timu yao.

MTIBWA

- Mbonde, Sabato, Kihimbwa (MSK)

Safu ya ushambuliaji inayoundwa na nyota hao imeanza vibaya katika mchezo wa kwanza baada ya kukubali kipigo cha bao 2 -1 dhidi ya Yanga lakini ilitulia na kuanza mambo kwa nyota wake kuonekana kuwa na uchu wa kufumania zaidi.

Stamil Mbonde, Kelvin Sabato ‘Kiduku’ na Salum Kihimbwa ndio mapacha watatu wa Mtibwa kwani nyota wote wana macho ya kuona nyavu. Safu ya ushambuliaji ya Mtibwa inayoundwa na nyota hao, waite MSK tayari ina mabao manne, Mbonde akiwa na mawili, huku wenzake wakiwa bado hawajatupia, lakini wakikaa sawa na wakiongezwa nguvu na Ismail Mhesa.

Wakata Miwa wa Manungu watatisha ligi ikisonga mbele. Kihimbwa na Kiduku rekodi zao za mabao msimu uliopita zinawabeba kama ilivyo kwa Mbonde.

Kwa kuwa ligi ndio kwanza imeanza na moto wa Mtibwa Sugar uliozoeleka miaka ya nyuma na kwa utatu huu, tutarajie makubwa kwani wapinzani watakuwa wanaokota tu mipira nyavuni.