Kuwaona Kagere, Makambo buku 7, mwanangu!

Muktasari:

Ubora wa washambuliaji wa Simba na Yanga mara nyingi mashabiki wanaupima zinapokutana timu hizo hasa pale anapofunga bao katika mechi ya watani

Dar es Salaam. Habari ya mjini kwa sasa ni washambuliaji wawili Meddie Kagere wa Simba na Heritier Makambo wa Yanga wawili hao wataonyeshana ubabe Septemba 30, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kiingilio cha Sh7000 tu.

Kagere amefunga mabao matatu katika Ligi Kuu akiwa anaongoza orodha ya wafungaji baada ya kucheza mechi tatu wakati Makambo amefunga bao moja katika mchezo mmoja aliocheza.

Uhodari washambuliaji hao ndiyo unaofanya mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga Septemba 30 kuwa na mzuka wa aina yake.

Mechi hiyo huteka hisia za wadau wengi wa soka kutokana na namna timu hizo mbili kuwa na ushindani pamoja na idadi kubwa ya mashabiki.

Katika kuhakikisha mashabiki wengi wanashudia mechi hiyo TFF imetangaza viingilio mapema VIP A, Sh 30,000, VIP B, Sh20, 000, viti vya Machungwa na Kijani 7,000.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia kwa Ofisa Habari wao, Clifford Ndimbo amesema, tiketi zitaanzwa kuuzwa mapema kuanzia Septemba 20.

"Mchezo wa Simba na Yanga upo kama kawaida na utachezwa siku iliyopangwa, mashabiki wajitokeze kwa wingi kwennda kushabikia timu zao," alisema Ndimbo.

Ndimbo aliongeza, katika mchezo huo wamezidisha ulinzi wa kutosha ili mashabiki waweze kuwa na amani muda wote wakiwa wanafuatilia mchezo huo.