Kumbe Mwakinyo ana rekodi kali tu kwenye ndondi!

Muktasari:

  • Tangu ameingia kwenye ndondi mwaka 2015, Mwakinyo amepigwa mara mbili tu na Akopian kwa pointi nchini Russia na Shaban Kaoneka hapa Bongo  kwa KO raundi ya sita mwaka 2015 lakini akalipa kisasi kwa Kaoneka mwaka mmoja baadae kwa kumchapa kwa KO raundi ya kwanza na hadi sasa ana rekodi ya kushinda mara 12 (8 kwa KO) na kupigwa mara mbili (1 KO).

Dar es Salam. Kama ulikuwa hujui bondia Hassan Mwakinyo hana rekodi kali na hiyo ya kumtwanga mzungu wa England Sam Eggington Technical Knock Out (TKO) ni mara ya kwanza, umepotea.
Basi bwana, jamaa ana rekodi za maana zipo kwenye kumbukumbu zake na vyama tofauti vya ngumi na hiyo ya mzungu si 'ishu' kabisa.
Tangu ameingia kwenye ndondi mwaka 2015, Mwakinyo amepigwa mara mbili tu na Akopian kwa pointi nchini Russia na Shaban Kaoneka hapa Bongo  kwa KO raundi ya sita mwaka 2015 lakini akalipa kisasi kwa Kaoneka mwaka mmoja baadae kwa kumchapa kwa KO raundi ya kwanza na hadi sasa ana rekodi ya kushinda mara 12 (8 kwa KO) na kupigwa mara mbili (1 KO).
Mwakinyo ana mkanda wa ubingwa wa WBA Pan Afrika ambapo alimchapa bondia wa Botswana, Anthony Jarmann kwa TKO raundi ya saba ya pambano ambalo pia lilikuwa la raundi 10, lilipigwa Gaborone.
Lakini, hadi anakuwa moto kwenye ngumi, Mwakinyo ana historia nzuri aliyoanza nayo nchini Russia ambapo alinyimwa mkanda wa Ubingwa wa Dunia wa WBC katika pambano lililofanyika Desemba 2, 2017 kwenye mji wa Moscow.
Katika pambano hilo, Mwakinyo alizichapa na Lendrush Akopian kuwania ubingwa huo kwa vijana katika uzani wa super feather pambano ambalo pia lilikuwa la raundi 10,  Mrusi alishinda kwa pointi.
"Pambano hili ndilo lilinipa funzo ukizipiga ugenini na kumaliza kwa pointi huwezi kushinda, kifupi ili ndilo lilinipa mzuka wa kushinda kwa KO nje ya nchi," alisema Mwakinyo.