Kocha wa Tunisia akimbia

Muktasari:

  • Klabu imeweka wazi kuwa hivi sasa wachezaji wake waliopo nchini Austria kujiandaa na msimu mpya wa ligi

Tunis, Tunisia. Kocha wa timu ya Taifa ya Tunisia, Nabil Maaloul, amebwaga manyanga na kukimbilia fedha za mafuta za klabu tajiri kutoka Qatari, Al Duhail.

Maaloul, atakayetimiza miaka 56 baadaye mwezi huu ameenda kuchukua nafasi ya Djamel Belmadi, ambaye ameacha kazi na inaaminika anasubiri kuteuliwa kuwa Kocha wa timu ya Taifa ya Algerian.

“Kocha wa timu ya Taifa ya Tunisia, Nabil Maaloul ndiye atakua kocha wetu ajaye,” ilisema taarifa ya klabu ya Al Duhail.

Klabu hiyo imeweka wazi kuwa hivi sasa wachezaji wake waliopo nchini Austria kujiandaa na msimu mpya wa ligi, wanaongozwa na nyota wao kutoka Tunisia, Youssef Msakni na kuwa Maaloul ataungana nao hivi karibuni.

Shirikisho la Soka Tunisia limeweka wazi kuwa limepokea na kukubali barua ya kujiuzulu ya Maaloul ambaye amedai kupata ofa nono kutoka klabu ya Al Duhail.

Kocha huyo aliiongoza Tunisi kucheza fainali za kwanza tangu mwaka 2006 na katika michezo mitatu iliyocheza chini yake ilipata ushindi katika mchezo mmoja ikiifunga Panama mabao 2-1.