Kocha Toto apania kurudi Ligi Kuu Bara

Mwanza. Kocha Mkuu wa Toto Africans, Almas Moshi amesema kikosi chake alichokisajili msimu huu ni lazima warudi Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Toto ilishuka daraja msimu uliopita na sasa inajiandaa na ligi daraja la kwanza inayotarajia kuanza Septemba 16 mwaka huu.

Toto imepangwa Kundi C pamoja na Pamba SC, AllianceFC, JKT Oljoro, Polisi Mara, Rhino Rangers, Transit Camp na Polisi Dodoma.

Kocha Moshi alisema kutokana na usajili alioufanya wa wachezaji mchanganyiko wazoefu na chipukizi ndio siri kubwa itakayoirudisha Ligi Kuu timu hiyo.

Alisema licha ya ugumu uliopo katika ligi daraja la kwanza, lakini hana wasiwasi na timu yoyote  kuwazuia kurudi Ligi Kuu.

Mjumbe wa Kamati Utendaji wa timu hiyo aliyehusika na suala la usajili, Keneth Emanuel alisema kuwa wachezaji waliojiunga na timu hiyo wote wako fiti.

Alisema kuwa kwa sasa kazi imebaki kwa benchi la ufundi kuongoza vijana hao kuhakikisha wanafanya vizuri na kurudi Ligi Kuu msimu ujao.

"Mimi kazi yangu ilikuwa ni kusajili na zoezi hili limeenda vizuri na jukumu lililobaki ni kwa benchi la ufundi tuna imani na vijana watafanya kweli" alisema Emanuel.