Kocha Prisons ambipu Mbelgiji wa Simba

PRISONS Mbeya ilimaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kwa kushika nafasi ya nne, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdallah Mohamed ‘Bares’ amesema anatamani msimu ujao wanyakue ubingwa unaoshikiliwa kwa sasa na Simba inayonolewa na Mbelgiji, Patrick Aussems.

Kocha Bares alisema anaamini kwa kikisi alichonacho na usajili waliofanya ana kila sababu ya kutwaa taji hilo ambalo klabu hiyo imekuwa ikilisikilizia hewani tu kutokana na kulowea jijini Dar es Salaam kwa miaka karibu 20 sasa.

‘’Kikosi nilichonacho kwa msimu huu ni zaidi ya kile cha msimu uliopita, wameondoka akina Mohamed Rashid, Eliuter Mpepo na wengine, lakini bado nina vijana tishio ambao wataweza kuhimili vishindo vya ligi hiyo,” alisema Bares.

Kocha Bora huyo alisema kumaliza kwao katika nafasi ya nne kwa msimu uliopita lilikuwa ni jambo lililokuwa katika mipango yao na msimu huu wanataka wavunje rekodi kwa kupindua meza dhidi ya Simba, Yanga na Azam zilizojimilikisha taji.

Bares alisema anataka kudhihirisha kushinda kwake tuzo ya Kocha Bora, kwa kuhakikisha anaivusha Prisons ilipokwamia msimu uliopita na kubwa ni taji la Vijana wa Msimbazi.