Kocha Masoud aibukia Uhuru kinyonge

Muktasari:

Mrundi huyo amekuwa katika wakati mgumu katika kikosi cha Simba tangu kutua kwa kocha Mbelgiji

Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma ameibukia kwenye Uwanja wa Uhuru kutazama mchezo wa Ligi Kuu baina ya African Lyon na Coastal Union unaoendelea.

Djuma ambaye hajaongozana na kikosi cha timu yake kilichopo Mtwara, kwa kile kilichotajwa kuwa kubaki jijini ili kuongoza programu ya wachezaji wa Simba ambao hawajasafiri kwenda Mtwara.

Kocha huyo ameonekana kuwa na utulivu wa hali ya juu kufuatilia mchezo huo akiwa amevalia miwani nyeusi huku mara kwa mara akiwa anachezea simu yake.

Djuma amechwa na wachezaji Yusuph Mlipili, Ally Salim, Rashid Juma, Abdull Selemani, Said Nduda, Asante Kwasi na Mzamiru Yassin pamoja na wale wa timu ya vijana.

Simba wanaingia katika mechi na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona huku wakiwa hawana rekodi ya kupoteza katika uwanja huo wala kufungwa na Ndanda tangu walivyopanda Ligi 2015.