Kiungo Mbeya City atimkia Sebria, Kocha Phiri njia panda

Mbeya. WAKATI kiungo Ayoub Semtawa ametimkia Serbia kucheza soka la kulipwa, Bodi ya Wakurugenzi ya klabu yake ya Mbeya City inatarajia kukutana wiki ijayo kujadili mambo mbalimbali likiwemo suala la Kocha Mkuu Kinnah Phiri.

Aidha Mbeya City imemuongeza mkataba beki wao Haruna Shamte ambaye atajiunga na kikosi chao siku yoyote kuanzia sasa, wakati kiungo Ayoub Semtawa ametimkia Serbia kucheza soka la kulipwa.

Chanzo makini ndani ya klabu hiyo kinasema kuwa kiungo huyo alieyevunja mkataba City baada ya kutopewa nafasi kikosini, ameenda kujaribiwa katika klabu moja ya nchini humo na taarifa zinasema anajiandaa kusaini mkataba.

Mbali  ya suala hilo taarifa zilizopo ni kwamba kocha huyo Mmalawi huenda akapewa mkono wa kwaheri kikosini.

City imekuwa kwenye maandalizi yao tya msimu mpya chini ya Kocha Msaidizi Mohamed Kijuso na leo Jumamosi itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Azam FC, mechi itakayochezwa uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Phiri mpaka sasa bado yupo kwao ikielezwa ana matatizo ya kifamilia na haijulikani atarudi lini, kitu kinachoifanya bodi huyo kujipanga mapema ili wasiharibikiwe.

Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe amesema hadi sasa wana mkataba na Phiri,lakini uamuzi ya kuendelea ama kutoendelea naye yataamuliwa na bodi yao.

"Ana mkataba ila kuna mambo yanakwenda ndivyo sivyo ambapo pia siwezi kuyaamua mwenyewe ni lazima bodi ikae na kujadili kwanza, bodi itakutana wiki ijayo na suala la Phiri litajadiliwa na kutolewa uamuzi," alisema Kimbe.