Oscar Joshua aeleza machungu ya kukaa nyumbani

Muktasari:

"Nafanya mazoezi kama niliyokuwa nafanya na timu, lakini hayana ushindani kwani naweka mwili wangu sawa, wakati nacheza ilikuwa kwa ushindani wa namba hadi kucheza kuisaidia timu yangu kupata mafanikio," anasema.

ALIYEKUWA beki wa Yanga, Oscar Joshua ametaja tofauti anayoiona kati ya kukaa nyumbani na kucheza ligi kuwa ni kushindwa kuwa kwenye ushindani wa juu, licha ya kufanya mazoezi kama kawaida huku akisema timu iliyosajili vizuri ina nafasi ya kufikia malengo yake.
"Nafanya mazoezi kama niliyokuwa nafanya na timu, lakini hayana ushindani kwani naweka mwili wangu sawa, wakati nacheza ilikuwa kwa ushindani wa namba hadi kucheza kuisaidia timu yangu kupata mafanikio," anasema.
Staa huyo kwa sasa anasema kuna mambo yake ya hapa na pale anayafanya ndiyo maana alikaa kando lakini anaweza akarejea wakati wa usajili wa dirisha dogo.
"Soka ni kazi yangu, iliyopo kwenye damu, ukifika wakati nitarejea kwenye majukumu yangu, ndiyo maana nafanya programu za mazoezi kama kawaida kwa sababu nazijua na najitambua kwamba natakiwa kufanya nini kipindi nilicho nje ya kazi," alisema.
Amezungumzia ligi ya msimu huu kwamba ina ushindani wa juu, kutokana uimara wa timu zinazocheza, huku akiwataka wachezaji kuonyesha uwezo utakaowapa burudani mashabiki wao.
"Ukisajili vizuri kuna kufanikiwa kutimiza malengo ya klabu, lakini pia inakuwa burudani kwa mashabiki kuona mpira wa ushindani wa juu, hii itakuwa ni hatua nzuri hata kwenye timu ya Taifa Stars, kuwa na wachezaji wenye uwezo wa juu," alisema.