Kili Stars yamshtua hadi Mwakyembe

Muktasari:

  • Waziri Mwakyembe aliyewapa kifyagio Zanzibar waliokuwa uwanjani jioni ya jana kuvaana na wenyeji Kenya katika fainali na kulikosakosa kombe kidogo tu, alisema kutolewa kwa aibu kwa Kili Stars ni somo kwa wadau wa soka.

KITENDO cha kikosi cha soka cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, kutolewa kwa aibu katika michuano ya Kombe la Chalenji huku Zanzibar Heroes ikifanya kweli kimemshtua Waziri wa Michezo Dk. Harrison Mwakiyembe.

Waziri Mwakyembe aliyewapa kifyagio Zanzibar waliokuwa uwanjani jioni ya jana kuvaana na wenyeji Kenya katika fainali na kulikosakosa kombe kidogo tu, alisema kutolewa kwa aibu kwa Kili Stars ni somo kwa wadau wa soka.

Waziri huyo alitoa kauli hiyo wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam wakati wa fainali michuano ya kibenki maarufu ‘Brazuka Kibenki’ iliyofanyika Uwanja wa Uhuru, ambapo alisema anaungana na Watanzania wote kuililia Kili Stars.

“Jamani Kili Stars basi sio ndo kila kitu, Taifa Stars inacheza vizuri tutajitahidi tu. Sio kama mmeumia pekee yenu wote tumeumia hapa, lakini bado tuna furaha kubwa kwa timu yetu nyingine ya Tanzania kufika fainali ya Chalenji.”

Waziri Mwakyembe alisema na kuongeza kuwa umefika muda uwakilishi wa mazoea wa Taifa Stars uangaliwe upya na kwa umakini ili iweze kufika mbali.

Katika michuano hiyo, benki ya DTB iliibuka kidedea baada ya kuifunga benki ya ABC kwa mikwaju ya penalti 3- 0 na kubeba zawadi kombe na medali.