Matola: Tumeondoa mzizi wa fitina Simba

Muktasari:

  • Kutokana na matokeo hayo, Simba imepunguza 'gepu' dhidi ya watani wao jadi, Yanga ambao wanawafuata kwa nyuma wakiwa na pointi 47 kabla ya mchezo wao wa leo Jumapili na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, ambapo walikuwa na mechi tatu mkononi.

UNAJUA kilichowatia hasira benchi la ufundi la Lipuli FC hadi wakahakikisha 'wanaibania' Simba katika mchezo wao jana Jumamosi na kumaliza kwa sare ya 1-1? Basi kwa taarifa yako ni zile kelele za mashabiki wanaodai wao ni Wekundu wa Msimbazi wakulialia.

Simba ambao ni vinara kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wanaongoza wakiwa na pointi 59, hakuna aliyetarajia kama wangetulizwa kwa sare hiyo na Lipuli hasa kipindi hiki wakiwa kwenye kasi na mzuka mkubwa wa kuwania ubingwa msimu huu wakidai kuwa timu hizo ni 'maswahiba' hivyo wangesaidiana.

Lipuli inafundishwa na makocha Amri Said na Seleman Matola ambao wote ni wachezaji na makocha wa zamani wa Simba walioitumikia timu hiyo kwa mafanikio makubwa.

"Unajua watu wanapenda kuzungumza, wengi wao wamekuwa wakituambia sisi ni Simba kwa sababu tumecheza huko na kufundisha, hawajui kuwa ile ni kazi tu kama nyingine, tulifanya kule na sasa tupo hapa," anasema Matola, ambaye alikuwa nahodha mwaminifu wa Simba.

Kwa matokeo hayo, Simba imepunguza 'gepu' dhidi ya watani wao wa jadi,  Yanga ambao wanawafuata kwa nyuma wakiwa na pointi 47 kabla ya mchezo wao wa leo Jumapili na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, ambapo mbali na huo wana mingine miwili mkononi.