Kazimoto awaamsha Kili Stars

Wednesday December 6 2017

 

By THOBIAS SEBASTIAN

KIUNGO mkongwe wa Simba, Mwinyi Kazimoto,  amewashtua wachezaji wa kikosi cha Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kinachoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Kenya kuwa kesho Alhamisi wasiwadharau Zanzibar Heroes .
Kazimoto amesema, alipokuwa na kikosi cha Kilimanjaro Stars  mara ya mwisho mwaka 2015,  katika michuano kama hiyo, walipoteza kwa kufungwa mikwaju ya penalti mitano kwa sita baada ya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
“Nakumbuka mimi ndio nilifunga katika mechi hiyo kabla ya Zanzibar kusawazisha lakini mechi ilikuwa ngumu na Zanzibar Heroes walicheza vizuri kuliko tulivyotarajia,”anasema Kazimoto .
“Mechi ya kesho dhidi ya Zanzibar Heroes ya Kili Stars, wasibeteke hata kidogo na kama watashangaa, watafungwa.”
Kili Stars itacheza kesho mchezo huo na Zanzibar Heroes ikiwa ni mechi ya pili kwao ya Kombe la Chalenji baada ya ile ya kwanza waliyotoa suluhu na Libya.
Kwa upande wa Zanzibar Heroes nao, ni mchezo wa pili baada ya kuichapa Rwanda mabao 3-1.