Kampeni TFF ruksa hadi asubuhi

Friday August 11 2017

 

By Mwanahiba Richard

Dodoma. Wagombea wamepewa nafasi ya mwisho kupiga kampeni hata kesho kabla ya upigaji kura kuanza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Uchaguzi huo, Wakili Revocatus Kuuli amewaambia wagombea kuwa, wapo huru kufanya kampeni zao hadi asubuhi ya kesho Jumamosi.

Uchaguzi huo unafanyika kwenye Ukumbi wa St Gasper mjini hapa huku ikidaiwa ajenda kuu katika mkutano mkuu ni uchaguzi mkuu pekee.

Akizungumza na MCL Digital, Kuuli alisema kampeni hizo wameruhusu zifungwe kabla ya shughuli ya uchaguzi kuanza saa 2:00 asubuhi.

Awali Kamati ya Uchaguzi ilitangaza muda wa siku tano wa kufanya kampeni hizo ambapo zilipaswa kufungwa leo Ijumaa saa sita usiku.

"Kila kitu kinakwenda sawa kabisa, tumeruhusu kampeni zifanyike hadi kesho asubuhi kabla ya kuanza uchaguzi, kampeni hizo ni zile za chini chini na utulivu mkubwa ili zisiingiliane na ratiba nyingine.

"Tutakapoanza taratibu zingine kama kuhakiki hapo ndio zitafungwa rasmi, kikubwa narudia kuwaomba wagombea na wapiga kura kuzingatia umakini kwani sheria zipo wazi," alisema Kuuli.

Wagombea 65 wapo mjini hapa tangu Jumatano wakitengeneza mazingira kwa wapiga kura huku kila mgombea akionekana anapambana kivyake kuomba kura na ulinzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ukiwa umeimarisha kila kona jambo ambalo linawapa hofu wagombea kufanya mambo tofauti na kanuni, taratibu na sheria za nchi.