Kagere awapagawisha mashabiki wa Simba Mwanza

Muktasari:

  • Wakizungumza na Mwanaspoti jijini hapa mashabiki hao wa Tawi Maarufu la Bendera Tatu walisema kwa kiwango kikubwa alichokionyesha straika huyo sasa hawana wasiwasi kwenye nafasi ya ushambuliaji ndani ya kikosi cha Simba.

Mwanza. Mashabiki wa Simba wa jijini Mwanza wameangalia kiwango cha mshambuliaji wao mpya Meddie Kagere katika mashindano ya Kombe la Kagame na kukubali muziki wake.
Mnyarwanda huyo ametua Simba akitokea katika Gol Mahia ya Kenya ambapo ameweza kuonyesha kiwango kikubwa kwenye Mashindano ya Kagame na kuipeleka timu hiyo kwenye fainali.
Wakizungumza na Mwanaspoti jijini hapa mashabiki hao wa Tawi Maarufu la Bendera Tatu walisema kwa kiwango kikubwa alichokionyesha straika huyo sasa hawana wasiwasi kwenye nafasi ya ushambuliaji ndani ya kikosi cha Simba.
Shabiki Hassani Kaheshi ambaye ndio kiongozi wa tawi hilo alisema mabosi wa timu hiyo wamefanya bonge la usajili kwa Straika huyo ambapo amesema ana kasi,nguvu na pia anajituma sana uwanjani.
“Kwanza ana kasi, nguvu na pia anajituma sana uwanjani huu ndio usajili ambao sisi mashabiki tunaoutaka na tunawapongeza sana mabosi wetu kwa kutuletea hiki kifaa”alisema Kaheshi.
Shabiki Jafari Abdul alisema  kwa kiwango alichokionyesha Kagere angalau sasa wanaweza kupumua kwa kuwa washambuliaji Emmanuel Okwi na John Bocco wamepata mbadala wao.
“Kama akiendelea na hii kasi yake basi tutakuwa tumepata mbadala wa akina Okwi na Bocco kwani msimu uliopita wachezaji hawa wakikosekana basi safu ya ushambuliaji inakosa makali”alisema Abdul.
Naye shabiki Husein Yahaya alisema kwa kasi ya Kagere alionyesha kwenye Michuano ya Kagame mabeki wa Ligi Kuu wanatakuwa na kazi nzito ya kuweza kumthibiti.