Kagera yamzuia Edo Christopher asisaini Coastal Union

Muktasari:

Edo mchezaji wa zamani wa Simba, tangu ajiunge na Kagera Sugar amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu.

 Dar es Salaam. Klabu ya Kagera Sugar iliposikia mshambuliaji wao, Edward Christopher anataka kutua Coastal Union ya Tanga, wakaona isiwe tabu 'fasta' wakaamua kukaa naye mezani na sasa atasaini  mkataba wa miaka miwili.

Coastal Union ilikuwa ikutane na mchezaji huyo wiki ijayo, Lakini Kagera Sugar wakawahi kumpiga pini na kufanya naye majadiliano ya kina na kufikia hatua ya kutaka asaini miaka miwili.

Mwanaspoti Online imemtafuta Edo ili afafanua ukweli juu ya jambo hilo, akasema: "Ni kweli nimefanya mazungumzo na Kagera Sugar , kifupi mazungumzo yetu yameenda vizuri na nitasaini muda wowote."

"Kwangu siwezi kuchagua timu kwa sababu kazi yangu ni soka, hivyo popote nafanya kazi ili mladi wanitimizie mahitaji yangu,"anasema Edo.