Julio akomalia katiba ya Simba

Muktasari:

Julio ambaye ni kocha wa timu ya Dodoma FC, amelalama kuwa vigezo vilivyowekwa kuwania nafasi za uongozi kwenye timu hiyo kitawanyima haki wanachama wengi wasio na elimu ambao wengi wao ndio walianzisha timu hiyo miaka mingi iliyopita.

Dodoma. Akiwa mmoja ya wagombea katika uchaguzi uliopita wa klabu yake ya Simba, Kocha na mwanachama wa klabu hiyo Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ amesikitishwa na kigezo kilichowekwa kwenye katiba mpya ya timu hiyo katika kugombea nafasi za juu za uongozi jambo ambalo alisema linakwenda kuwaweka kando wanachama maskini na wasio na elimu.
Julio ambaye ni kocha wa timu ya Dodoma FC, amelalama kuwa vigezo vilivyowekwa kuwania nafasi za uongozi kwenye timu hiyo kitawanyima haki wanachama wengi wasio na elimu ambao wengi wao ndio walianzisha timu hiyo miaka mingi iliyopita.
“Mfumo mpya ambao umepitishwa ni mzuri ila naona unaenda kuondoa thamani ya wanachama maskini na wasio na elimu kupata haki yao ya kuwania nafasi za uongozi ndani ya timu yao. Unajua hao ndio walianzisha timu na matokeo yake kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo matabaka baina ya wanachama,” alisema Julio.
Kocha huyo mwenye mbwembwe, aliongeza kuwa kama wanachama walipata nafasi ya kukipitia na kuelewa kipengele cha elimu kugombea nafasi za Uongozi.
Pia wakakubaliana nacho, hana kinyongo ila hofu yake ni kama walinogewa na mengine mazuri kwenye katiba hiyo wakasahau kipengele hicho muhimu kinachoondoa haki ya mwanachama asiye na elimu.
“Hofu yangu ni hapakuwa na kupangwa kwa baadhi ya wanachama na kujibu ndiyo kwenye kipengele cha elimu au mazuri mengi yaliyomo katika mfumo mzima wa mabadiliko ulisababisha wasiwe na shaka na kipengele cha elimu  kubwa ndio uwe kiongozi kwenye timu kwa sababu tusio na elimu tutakosa haki hiyo,” alisisitiza Julio.
Katika hatua nyingine, Julio aliungana na wanachama wote wa Simba kukubaliana na mabadiliko mapya kwenye timu hiyo.
Akisema huo ni mwanzo wa mafanikio ya timu yao na zaidi ana matumaini makubwa na mwanahisa mkuu Mohammed Dewji ‘Mo’ kutokana na mchango wake mkubwa wa kuirejeshea makali timu hiyo baada ya miaka 5.