Joel Bendera afariki dunia

Muktasari:

Bendera aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Stars pekee iliyoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 1980 kule Nigeria, amekumbwa na mauti hayo masaa manne tu tangu alipofikishwa Muhimbili akitokea mjini Bagamoyo.

KOCHA wa zamani wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Joel Nkaya Bendera,  amefariki dunia jioni hii ya leo Alhamisi katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Bendera aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Stars pekee iliyoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 1980 kule Nigeria, amekumbwa na mauti hayo masaa manne tu tangu alipofikishwa Muhimbili akitokea mjini Bagamoyo.
Msemaji wa Hospitali ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha, amethibitisha kifo cha mwanamichezo huyo maarufu, ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge (Korogwe Mjini), Naibu Waziri wa Michezo, Habari na Utamaduni. Pia amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa (Morogoro kisha Manyara).
"Ni kweli Joel Bendera amefariki. Aliletwa leo saa 6:30 kwa gari la wagonjwa akitokea Hospitali ya Bagamoyo, ilipofika saa 10:24 jioni alifariki,” amesema Aligaesha.
Mwanaspoti  ilipotaka kujua chanzo cha kifo chake, alisema: “Hilo ni suala la familia, lakini kwa wakati huu itoshe kusema amefariki.”
Katika mabadiliko ya wakuu wa mikoa yaliyofanywa na Rais John Magufuli Oktoba 26, Bendera alikuwa miongoni mwa wakuu wa mikoa waliostaafu na nafasi yake imechukuliwa na Alexander Mnyeti aliyepandishwa kutoka Mkuu wa Wilaya ya Arumeru.