Jide ambeba Domo Kaya

Muktasari:

Domokaya akiwa na mwenzake Man Dojo waliwahi kutamba na vibao mbalimbali kikwemo ‘Nikupe nini’ na ‘Dingi’ lakini kwa muda mrefu wamepotea katika gemu.

UNAKUMBUKA ile chama ya Domo Kaya na Man Dojo? Basi msanii wa Bongo Fleva, Judith Wambura’Lady Jay Dee’, amemuibua Domo Kaya na anataka amsindikie katika onyesho lake ‘Anaweza Consert’ litakalofanyika Machi 21 Jijini Dar es Salaam.

Domokaya akiwa na mwenzake Man Dojo waliwahi kutamba na vibao mbalimbali kikwemo ‘Nikupe nini’ na ‘Dingi’ lakini kwa muda mrefu wamepotea katika gemu.

Akizungumza na jana alipotembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, ambao ni wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, Citizen na Mwanaspoti, Jay Dee au ‘Jide Commando’ alisema ameamua kumshirikisha msanii huyo kwa kuwa ni kati ya watu ambao amekuwa akifanya nao kazi kwa muda mrefu.

Aliwataja wasanii wengine watakaokuwepo ni Bushoke, Nick Mbishi, na Alan Junior, ambapo watu zaidi ya 300 wanatarajiwa kuhudhuria.

Akitaja sababu ya kwenda kufanya onyesho hilo hoteli ya Golden Tulip, Jide ambaye kwa jina lingine anajulikana kama Komando, alisema ni kutokana na kuwa na uwanja mkubwa wa kubeba watu wengi kwa wakati mmoja.

“Unajua hii itakuwa ni mara yangu ya pili kufanya onyesho ndani ya mwaka huu, kwani la kwanza nililifanyia Hoteli ya Serena na lilihitajika kuwa na watu wasiozidi 50 lakini hili kwa kuwa litakuwa na watu wengi ndio maana nikaamua kufanyia katika hoteli hiyo,”alisema.

Lady Jay Dee ambaye leo pia anatarajia kuitambulisha rasmi ngoma yake ya ‘Anaweza’, na mpaka sasa ameshatoa albamu saba na mwaka alioziachia kwenye mabano, Machozi (2000), Binti (2003), Moto (2005), Shukrani (2007), The Best of Lady Jaydee (2012), Nothing But The Truth (2013) na Woman (2017).