Jezi ya Messi yampa mzuka Kaheza

Wednesday June 13 2018

 

By DORIS MALIYAGA

HIVI unajua kuwa straika mpya wa Simba, Marcel Kaheza 'Rivaldo' anafurahi sana anapokuwa anacheza akiwa amevaa jezi namba 10 na baada ya Wekundu hao kumkabidhi, amesisitiza ataitendea haki.
Kaheza ambaye anarudi Simba kwa mara pili, ni mpenzi wa jezi namba hiyo kwa sababu ndiyo ilikuwa inavaliwa na nahodha wa zamani wa Brazil, Rivaldo Vítor Borba Ferreira ambaye ni mchezaji anayempenda zaidi duniani.
Aliitumia namba 10 alipokuwa anacheza timu ya vijana lakini alipopandishwa kucheza ya wakubwa ilikuwa inatumiwa na Mzambia Felix Sunzu jambo lilimfanya apewe namba 32 na alikuja kurudishiwa baadaye.
amesema: "Nimefurahi kurudi Simba na kukabidhiwa tena jezi namba 10 kwani nnaipenda sana. Na kutokana na hilo naamini itaniongezea morali wa kupambana ili niitendee haki kama unavyojua namba ya jezi hii inavaliwa na watu wazito,"alisema Kaheza.
Amesema, changamoto kubwa aliyonayo sasa ni kuona kwa namna gani anaingia kucheza kikosi cha kwanza bila matatizo.
Kaheza aliitumia pia jezi namba 10 alipopelekwa kwa mkopo kwenye timu ya Majimaji ya Songea ambayo amemalizana nayo msimu uliomalizika.