JKU, yazichonganisha Yanga, Singida kwa Feisal

Muktasari:

  • Mchezaji yeyote ambaye hajamaliza mkataba au mkataba wake haujasitishwa na klabu yake, au ambaye hajamaliza msimu atakaposajiliwa na klabu nyingine ni lazima ahamishwe kuanzia ngazi ya klabu.

Dar es Salaam. Mabingwa wa Zanzibar, JKU wamekata mzizi wa fitina baada ya kutangaza  mchezaji wao Feisal Salum 'Fei Toto' ni mali halali ya Yanga huku wakiwataka mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara 27 kukaa mezani na Singida United ili kumaliza sintofahamu juu ya usajili wa kiungo huyo.
JKU wametoa uthibitisho huo saa chache baada ya Yanga kumtangaza na kumtambulisha kiungo huyo baada ya kumsainisha mkataba wa miaka miwili huku tayari akiwa alishasaini mkataba wa kuichezea Singida United wiki kadhaa zilizopita.
Katibu Mkuu wa JKU, Saadu Ujudi alisema hakuna haja ya Singida United kulalamika kwenye vyombo vya habari na badala yake wanapaswa kulimaliza suala hilo kiungwana kwa sababu kiungo huyo ni mchezaji halali wa Yanga.
Sisi JKU tumeshapata fedha zetu za fidia ya kuvunja mkataba kutoka kwa Yanga. Kuhusu hilo suala la Singida United sisi halituhusu kwa sababu wao walimalizana na mchezaji wakati walikuwa wanafahamu wazi kuwa ana mkataba na JKU. Na kwa upande wetu kwa kuwa hilo ni suala la mtoto wa shangazi na mjomba, naamini watakaa chini kumalizana wenyewe ila sisi tunachofahamu ni kwamba Feisali ni mchezaji halali wa Yanga," alisema katibu huyo wa JKU.
Hata hivyo Singida United wamemjia juu kiungo huyo kwa kitendo chake cha kusaini Yanga huku akiwa tayari ameshasaini mkataba wa kuichezea timu yao na kudai kuwa watampeleka mbele ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili wapate haki yao.
Sisi kama Singida United tumemsajili kwa mkataba wa miaka mitatu, tukiwa tumekutana naye chini ya mwanasheria na wakala wake. Mchezaji amesaini mkataba wa kuitumikia Singida kwa miaka mitatu na sehemu kubwa ya fedha ameshachukua na sio mkataba wa awali kama watu wanavyodhani.
“Ule ni mkataba kati ya Singida United na mchezaji ambayo inatambulika na kimsingi ndio itakayotumika katika usajili wake kama endapo tutakuwa tumefikia makubaliano ya kumsajili pale ambapo TFF wataamua vinginevyo," alisema Sanga.
Kanuni ya 66 usajili kipengele cha Katazo inasema: Haitaruhusiwa kwa mchezaji yeyote kutia saini mikataba ya klabu zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Mchezaji atakayesaini mikataba ya klabu mbili tofauti kwa wakati mmoja atafungiwa kucheza mpira wa miguu kwa mashindano yoyote rasmi kwa kipindi cha mwaka mmoja.