JICHO LA MWEWE: euri ya akina Maguli itazidi kutupa jeuri

SAHAU kuhusu matokeo ya Kilimanjaro Stars ya juzi Jumamosi pale Kenya kwa kuwa, tumejitakia. Himid Mao Mkami amefuzu majaribio katika klabu moja ya Afrika Kusini. Wakati nikitegemea habari zaidi kuhusu Himid, ghafla nikasikia Elias Maguli amesaini mkataba wa kukipiga katika klabu ya Polokwane City pale pale Afrika Kusini.

Siku chache awali, Simon Msuva, alikuwa amechaguliwa katika kikosi cha mwezi katika Ligi Kuu ya Morocco. Hapo hapo Farid Mussa anafanya vema Hispania na Mbwana Samatta ameanza mazoezini mepesi baada ya operesheni ya goti pale Ubelgiji. Abdi Banda ni panga pangua Baroka.

Imeanza kuwa kitu cha kawaida siku hizi. Kusikia habari za mastaa wetu wanaocheza ugenini. Ikanikumbusha kitu fulani cha miaka ya nyuma. Zamani tulinyanyasika sana wakati Taifa Stars ilipokuwa inakaribia kucheza mechi yoyote ya kimataifa katika ardhi ya nyumbani.

Iwe Malawi, Zambia, Zimbabwe, Uganda, Benin au wengineo, vichwa vya habari vilikuwa vinatutisha tu. Ungeweza kusoma ‘Zambia yawasili na mastaa sita wa kulipwa’. Wengine wangeandika ‘Malawi kuwasili leo na nyota tisa wa kulipwa’. Mwingine angeandika ‘Benin kuwasili kesho, mastaa wao wa kulipwa kuwasili keshokutwa’.

Hii ndio ilikuwa mikwara ya magazeti yetu siku za nyuma. Mara kadhaa tulijikuta tuna hofu kubwa kabla hata mechi haijaanza. Wachezaji wetu wote wa timu ya taifa wanaoanza mechi walikuwa wanacheza hapa hapa nchini. Ilikuwa kama vile tumepigwa marufuku kuwa na wachezaji wa kulipwa nje ya nchi.

Kitu kilichokuwa kinaniumiza sana na pale unapokwenda uwanjani kutazama mechi yenyewe. Unagundua kuwa Mrisho Ngassa anakuwa mchezaji bora uwanjani. Unagundua kuwa kiungo wa Malawi tuliyeambiwa anacheza Bidvest ya Afrika Kusini sio bora sana kuliko Athuman Idd ‘Chuji’.

Tofauti yetu na wao ilikuwa moja tu, wenzetu walikuwa kama sisi, na sisi tulikuwa kama wao, lakini wenzetu walikuwa wameondoka katika nchi zao na kwenda kucheza nje. Sisi tulikuwa tunafikia viwango hivyo na tuliamua kubaki hapa hapa.

Nchi ambayo wachezaji wa Zimbabwe, Malawi, Zambia, Msumbiji walikuwa wanaionea sana na Afrika Kusini. Na ndio nchi ambayo wachezaji wetu sasa wanaonekana kuvumbua chaka lao kwa nguvu zote.

Leo wachezaji wetu wanazidi kwenda nje na wanacheza. Hawakai benchi. Huwa ninanikumbusha kitu ambacho nilikuwa naamini kwamba, wachezaji wetu walikuwa na uwezo wa kucheza katika nchi zile zile ambazo tulikuwa tunatishwa kusikia wachezaji wa timu nyingine za taifa wakicheza.

Kama Ibrahim Ajib ameamua kucheza Yanga ni kwa sababu ameamua tu na sio kwamba, hawezi kucheza Bidvest au Esperance. Hatuna tunachoweza kumfanya. Hatuwezi kuweka tundu la bastola katika shingo yake. Ni maamuzi yake.

Wachezaji wetu walioamua kuchukua fursa kila inapojitokeza, kama hawa akina Maguli ndio maana watatufanya tunuse Afcon kwa mara nyingine baada ya miaka takribani 40 tangu tucheze mara ya mwisho pale Nigeria.

Kuna kitu tofauti wanakipata wanapokwenda kucheza nje. Zaidi ya yote ni kwamba wanaongeza uwezo wa kujiamini pindi wanapocheza na timu mbalimbali za Afrika.

Lakini, pia kuna kitu ambacho kinajengeka katika jamii yetu ambayo awali ilijaa watu wasiojiamini. Kuna kizazi kipya kinachokuja ambacho kitawatazama zaidi akina Samatta na Maguli na kuamua kufuata nyayo. Nyakati hizi TFF inahitaji kocha makini, ambaye ana utaalamu mkubwa zaidi wa soka kwa ajili ya kutufikisha mbali. Kuna wachezaji waliopo katika Ligi wanaweza kuunganishwa na wachezaji wetu wanaocheza nje wakatupatia kitu.

Wachezaji wapo lakini suala la kocha bado tunapiga cheng.

Hawa akina Maguli, Samatta, Farid, Banda na wengineo wamefunguka macho wakati Taifa likiwa limeinamisha kichwa chini.