Huu mkwara wa Mtaka sio wa mchezo

Muktasari:

Mtaka ametamka hayo ikiwa ni siku chache tu kabla ya uongozi wa RT kukutana na waandaaji wote wa mbio, mkutano unaotarajiwa kufanyika keshokutwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

RAIS wa Shirikisho la Riadha la Tanzania (RT) ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, ana mikwara usipime.

Bosi huyo wa wafukuza upepo ametoa vigezo kwa waandaaji wa mbio zote unazozijua ambazo zinafanyika hapa nchini huku akasisitiza wanaoandaa mbio bila kufuata kanuni kuwa kuanzia sasa wakome.

Mtaka ametamka hayo ikiwa ni siku chache tu kabla ya uongozi wa RT kukutana na waandaaji wote wa mbio, mkutano unaotarajiwa kufanyika keshokutwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umeitishwa ili waandaaji hao wakabidhiwe kanuni mpya za riadha na unatarajiwa utahudhuriwa pia na wadhamini, mwanariadha, Alphonce Simbu na Kampuni ya MultChoice Tanzania (DSTV).

“Kuna uibukaji mkubwa wa watu kuandaa ovyo riadha, kuanzia sasa ni lazima taratibu zifuatwe,” alisema.

“Kuna taratibu za uandaaji wa matukio ya riadha, viwango vya matukio hayo, pia mpishano wa tukio moja na jingine bila kuingiliana katika kalenda.”