Hesabu kali! Simba, Yanga jipangeni

Muktasari:

Kwa sasa Mkoa wa Mbeya unawakilishwa na timu za Mbeya City na Tanzania Prisons na uongozi wa Chama cha Soka mkoani hapa, MREFA, umeziangalia kwa makini timu hizo na kukubaliana kufanya jambo moja la maana.

VIGOGO wa soka mkoani Mbeya sio wa kuchezea kabisa unaambiwa, na kama mikakati yao itakwenda kama walivyopanga basi Simba, Yanga na Azam itabidi zijipange kwelikweli.

Kwa sasa Mkoa wa Mbeya unawakilishwa na timu za Mbeya City na Tanzania Prisons na uongozi wa Chama cha Soka mkoani hapa, MREFA, umeziangalia kwa makini timu hizo na kukubaliana kufanya jambo moja la maana.

Iko hivi. MREFA wamekubaliana kwamba kila mwaka kuhakikisha wanapandisha timu moja kutoka daraja moja hadi lingine ili kurejesha makali ya soka mkoani hapa.

Mbeya ina timu za madaraja yote kuanzia la nne, tatu, pili, la kwanza na Ligi Kuu Bara, ambapo sasa wanataka kuja kivingine kwa kuwa vipaji vya kutosha vipo kila kona.

Katika Ligi Daraja la Tatu Mkoa wa Mbeya unawakilishwa na Bingwa wa Mkoa, Tukuyu Stars, Daraja la Pili inawakilishwa na Ihefu FC ya wilayani Mbarali, wakati daraja la kwanza inawakilishwa na timu mbili za Boma na Mbeya Kwanza.

Mwenyekiti wa MREFA, Elias Mwanjala alisema uongozi wake mpaka sasa katika vipindi viwili wamezipandisha hadi Ligi Kuu Bara klabu za Mbeya City na Tanzania Prisons, kadhalika, Mbeya Kwanza, Boma, Ihefu na Tukuyu Stars.

“Tunataka kufanya mambo ya maana kwa haraka zaidi, hatutaki kuona timu zinapanda na kushuka daraja linatokea tena hapa Mbeya. Tumejiwekea dhamira na mikakati ya maana kuwa, kila mwaka timu inayopanda daraja kutoka hatua moja kwenda nyingine haishuki bali inasonga mbele zaidi,” alisema Mwanjala.

Alisema hatua ya Mbeya kuwa na timu zaidi ya moja kwenye ligi zote zinazotambulika na TFF ni ishara kwamba, soka linazidi kusonga mbele na kukuza vipaji na kutoa ajira za uhakika kwa vijana.