Heinken yawapa mzuka mashabiki Fainali Ulaya

USIKU wa jana ulikuwa na balaa kwa upande mmoja huku mwingine ukiwa na mzuka mwingi kwelikweli. Ndio, mashabiki wa Liverpool walienda kulala huku wakiwa na hasira na kipa wao, Loris Karius ambaye aliruhusu kupigwa bao mbili za kizembe na kuipa Real Madrid taji la tatu mfululizo la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika fainali hiyo matata kabisa iliyopigwa uwanjani Olympic jijini Kiev, Ukraine, Liverpool ililala kwa mabao 3-1 huku supastaa wa Wales, Gareth Bale akitupia nyavuni mabao mawili matata kabisa huku moja likiwa na shuti kali la ‘hapa na Bagamoyo’ ambalo lilimshinda Karius na kutinga wavuni na kufuta kabisa matumaini ya Majogoo wa Anfield kupambana.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa soka na watu maarufu jijini Dar es Salaam, walipunguza stress zao kidogo baada ya kukusanyika kwenye klabu za Red Sea Arena, George & Dragon na Club 777 kuangalia burudani hiyo wakikutanishwa pamoja na bia ya Heineken.
Zaidi ya mashabiki 2,600 nchini walifurahia fursa ya kipekee ya kutazama fainali hizo katika mazingira safi na tulivu huku wakishuhudia Liverpool wakilala kiulaini kabisa ndani ya dakika 90 za mchezo.
Heineken ni mmoja wa wadhamini wakuu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo ikafanya jambo la maana kuwalete pamoja mashabiki ili kunogesha fainali hiyo ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Meneja wa Heineken Afrika Mashariki, Njeri Mburu alisema: “Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ni moja kati ya ligi zinazohusisha wachezaji wakubwa. Timu zote bora Ulaya zinashiriki ligi hii hivyo, bia ya Heineken inayojulikana na kutumiwa na watu wengi duniani kutokana na kuwa na uhusiano wa karibu.
“Mwaka huu, wateja wetu sio tu hawatafurahia kutazama ligi bali pia kushiriki fursa zinazokuja na ligi. Tuko hapa kufurahi na kubadilishana taarifa kuhusiana na michuano hiyo.”