He! Mwaikimba bado tu

UNAMKUMBUKA Gaudence Mwaikimba? Ndio yule straika matata wa zamani wa Yanga, sasa kwa taarifa yako jamaa bado analipiga gozi la ng’ombe na msimu ujao atakuwa akichana nyavu kwenye Ligi Daraja la Kwanza akiwa na Boma FC.

Mwaikimba ambaye mara ya mwisho alionekana msimu wa 2014/15 akikipiga Azam FC, kisha akapotea hadi mwaka jana alipoibukia Boma FC iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Pili na kufanikiwa kuipandisha ngazi msimu ujao.

Mbali na Mwakimba, pia straika mwingine Six Mwasekaga ambaye ameshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu akiitumikia Majimaji kabla ya kutimuliwa klabuni hapo kwa utovu wa nidhamu, naye ataungana naye kukipiga klabuni hapo kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020.

Mwasekaga ameliambia Mwanaspoti kuwa kutokana na Boma FC kuwa ya nyumbani kwao Kyela, hawana budi kuonyesha uzalendo ili kusaidia kuipandisha kucheza Ligi Kuu Bara hapo baadaye.

‘’Ni lazima tukae na kufikiria tukiendelea kuiacha timu hii na kuzitumikia za mikoa mingine nani atajitolea kuipandisha daraja, hapa ni lazima kuonyesha uzalendo. Sisi ndio vijana wa Kyela ni lazima tupambane?” alisema Mwasekaga.

Boma itaungana na Mbeya Kwanza yenye maskani yake jijini hapa kuuwakilisha Mkoa wa Mbeya kwenye michuano ya Ligi Daraja la Kwanza kwa msimu ujao.

Msimu huu timu sita za ligi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini zilipanda daraja kucheza Ligi Kuu.