He! Himid akomalia ubingwa

Tuesday April 10 2018

 

By OLIPA ASSA

LICHA ya Azam FC kuendelea kukwama kwenye mbio za ubingwa baada ya kulazimishwa sare na Mbeya City, lakini bado nahodha wake Himid Mao amesema wana nafasi ya kubeba taji hilo msimu huu.

Himid, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa viungo bora kwa sasa, huku akijiamini alisema wamebakiza mechi ngumu dhidi ya Yanga na lolote linaweza kutokea, hivyo wamejipanga kupambana mpaka kieleweke.

“Simba kuongoza ligi haina maana ligi imefika mwisho wa safari, hii ligi bado ngumu na hilo ndilo linatufanya tuendelee kupambana bila kuangalia nyuma ambako tulikwama baada ya mechi,” alisema.

Himid ambaye ni mtoto wa kiungo wa zamani wa kiungo Pamba ya Mwanza, Mao Mkami alisema ikitokea hawajapoteza mechi zilizosalia, basi watakuwa wanaziombea dua mbaya Simba na Yanga ili zipoteze michezo yao ili mwishoni mwa msimu wapeleke ndoo Chamzi.

“Ubingwa ni kama ngazi bado tunapanda, Simba na Yanga nazo zinaendelea kupanda, hatuwezi kushuka kwa hofu za kelele zao za kujitanguliza kana kwamba wameishamaliza wakati bado wana mechi ya kukutana wenyewe kwa wenyewe,” alisema na kuongeza: “Niwapongeze Mbeya City kwa kuonyesha uwezo dhidi yetu, wakiendelea hivyo katika mechi zilizosalia watafika mbali,”alisema Himid.