Hata makocha uvaaji saa wanauthamini

Muktasari:

  • Hatukuwa na televisheni wala simu za mkononi. Niliwahi kuzungumza na mwandishi nguli Freddy Macha akanisimulia alivyomwona Diego Maradona akicheza uwanja maarufu wa Maracana kule Brazil, 1988. Mtangazaji mashuhuri Tido Mhando aliwahi kutusimulia alivyowaona wachezaji wetu wasifika kina Maulidi Dilunga na Abdallah Kibaden.

SIKU hizi kila mwanadamu analofanya linaangaliwa sana kuliko zamani. Tukichukulia michezo, zamani Tanzania tulisikia tu majina ya wachezaji kama Bobby Moore, George Best, Pele na Diego Maradona. Tuliwasikia redioni, magazetini na mara moja moja kupitia ndugu au marafiki waliosafiri ugenini. Hatukuwa na televisheni wala simu za mkononi. Niliwahi kuzungumza na mwandishi nguli Freddy Macha akanisimulia alivyomwona Diego Maradona akicheza uwanja maarufu wa Maracana kule Brazil, 1988. Mtangazaji mashuhuri Tido Mhando aliwahi kutusimulia alivyowaona wachezaji wetu wasifika kina Maulidi Dilunga na Abdallah Kibaden.

Leo teknolojia ya mitandao, simu za mkononi na runinga zenye idhaa zaidi ya 40 vinatuletea kila aina ya habari. Maendeleo ya habari na urushaji taarifa yako juu sana sasa.

Kutokana na mtazamo huu juzi nilikuwa nikitafakari kuhusu habari iliyochapishwa na gazeti moja la hapa Uingereza.

Habari ilitathmini aina na thamani ya saa wanazovaa makocha wa Ligi Kuu England. Tathmini ilinikumbusha majadiliano fulani yanayoendelea mtandao wa Instagram kuhusu simu ya tajiri zaidi kuliko wote Afrika bilionea Aliko Dangote. Wadau walibishana na kuulizana bei na aina ya simu ya Dangote.

Hilo ndilo lililozungumziwa kuhusu makocha wa Premier Ligi. Saa ya bei ya juu ni ya kocha wa Burnley -timu isiyofahamika sana Afrika Mashariki.

Kocha huyo Sean Dyche huvaa saa yenye thamani ya Paundi 45,000 ukilinganisha na ya Pep Gurdiola ya Pauni 1,900 au Arsene Wenger Paundi 8,350. Hata hivyo, lengo si tu bei bali umaana wa saa hizi. Saa ya Pep Guardiola wa Man City- aina ya Cimier QNET city- inaweza kuwa chee, lakini ilitengenezwa maalumu kuonyesha mwaka klabu hii ilipobuniwa. Saa hutengenezwa chache (1,880) kuadhimisha mwaka 1880 Man City ilipoanzishwa.

Mauzo ya saa anayovaa Arsene Wenger - IWC Aquatimer- hutumika kusaidia kuendeleza maisha na viumbe vya visiwa vya Galapagos vilivyoko Marekani ya Kusini karibu na Ecuador. Visiwa hivi vinavyosifika kwa mimea na viumbe wakuvutia kama kasa na kobe viko hatarini kutoweka kutokana na uharibifu wa kimazingira na tufani la mara kwa mara.

Mbali na umaana pia kuna utengenezaji wa hali ya juu. Mnunuzi unapotaka kununua saa aina ya Rolex Daytona anayovaa kocha Aitor Karanka aliyekuwa (Middleborough) inabidi ujipange katika foleni na itakuchukua miaka miwili hadi uipate. Saa hii inagharimu Pauni 10,000. Kwa hiyo si tu ya kwenda dukani na kulipa.

Saa za Rolex zinathaminiwa zaidi na matajiri. Rolex Cosmograph Daytona inayovaliwa na Kocha Tony Pulis wa West Brom ilipendwa sana, mshambuliaji mashuhuri wa Cameroon Samuel Eto’o.

Cameroon ilipoingia Kombe la Dunia la 2010, Eto’o alimzawadia kila mchezaji saa hiyo ambayo gharama yake ni Pauni 15, 950.

Saa nyingine ya Rolex Oyster Perpetual anayovaa Walter Mazzarri aliyekuwa Watford, ni ya Paundi 4,000 (bei rahisi ukilinganisha na za wenzake), lakini imekuwa kipenzi cha marais mbalimbali wa Marekani kama Dwight Eisenhower 1953-61 na Ronald Reagan – 1981-89.

Saa ya bei rahisi kuzidi zote ambayo sisi wadau tunaweza kubahatisha bahatisha inagharimu Paundi 40 (kama laki moja za Bongo) na ilivaliwa na Rais zamani wa Marekani Bill Clinton na kocha Bob Bradley aliyekuwa Swansea City hadi miezi michache iliyopita akatimuliwa.