Haruna ashusha wawili Msimbazi

Tuesday November 14 2017Haruna Niyonzima

Haruna Niyonzima 

By THOBIAS SEBASTIAN

DIRISHA dogo la usajili kwa Ligi Kuu Bara linafunguliwa kesho Jumatano na habari za moto ambazo Mwanaspoti imejiridhisha nazo ni kwamba Simba tayari ina majina mawili mapya mezani. Pia ua mmoja atasaini.

Majina hayo ni ya wachezaji wa kigeni kutoka Rwanda anakotokea kiungo mahiri, Haruna Niyonzima. Wachezaji hao ni kiraka Muhire Kelvin ambaye ana uwezo zaidi wa kucheza namba kumi ameng’ara na klabu ya Isonga, akaibukia Rayon Sport na baadaye Shakhtyor Soligorsk ya Belarus.

Muhire alizaliwa Oktoba 17, 1998 na amecheza timu ya Taifa ya vijana ya Rwanda chini ya miaka 23. Kifaa kingine ambacho Simba wanakiwinda ni Shasir Nahimana mwenye uwezo mkubwa wa kufunga na amekuwa moja ya wachezaji nyota kwenye Ligi Kuu Rwanda akiichezea Rayon Sport.

Nahimana ambaye amezaliwa Agosti, 1993 anavaa jezi namba kumi na huenda Simba walimuona katika mechi ya kirafiki ambayo walicheza Dar es Salaam Simba Day, lakini kama haitoshi aliwafunga Azam bao moja kwenye mechi ya kirafiki iliyochezwa Rwanda Julai 8, 2017.

Mmoja wa viongozi wa Simba aliiambia Mwanaspoti kwamba Kocha Msaidizi, Masoud Djuma, amewahakikishia wachezaji hao wana uwezo kuliko baadhi ya mastaa wa kigeni walioko Simba kwa sasa.

Ujio wa wachezaji hao unaamaanisha wakisajiliwa basi wachezaji wawili wa kigeni wataenda na maji Msimbazi huku Mghana, Nicolaus Gyan na Mrundi, Laudit Mavugo wakitajwa. Mavugo anatajwa kujiunga na Gor Mahia ya Kenya na huenda akaondoka hata kabla ya maandalizi ya Krismasi hayajaanza kama mambo yatakwenda sawa.