Hapo kwa Chirwa na Ajibu ndiyo penyewe unaambiwa

Muktasari:

Akili ya kocha wa timu hiyo, George Lwandamina, kwenye matumizi ya Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu imekubalika kwa wakuu wake wa kazi.

YANGA imeweka kambi ya muda hapa Tabora ikijiandaa kuelekea Shinyanga kucheza na Stand United. Akili ya kocha wa timu hiyo, George Lwandamina, kwenye matumizi ya Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu imekubalika kwa wakuu wake wa kazi.

Iko hivi, katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar ambao Yanga ilishinda mabao 2-1, Lwandamina aliwatumia Ajibu na Chirwa eneo la washambuliaji wa kati na wawili hao walionyesha uwezo mkubwa wakifanya mambo mawili muhimu yanayofanana.

Chirwa ndiye aliyefunga bao la kwanza lakini pasi ya bao hilo ilitengenezwa kiufundi na Ajibu. Pasi hiyo iliyowapoteza mabeki wa Kagera ilichongwa na mguu wake wa kulia huku Chirwa naye akimalizia kwa mguu kama huo.

Ajibu naye alifunga bao la pili katika kipindi cha pili kwa akili kama hiyo akipiga shuti la hesabu lililokwenda nyavu ndogo akitumia mguu wake wa kulia, lakini pasi ya bao hilo ilitengenezwa na Chirwa akitumia mguu wa kulia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga Hussien Nyika amesema: “Nimefurahishwa na safu hii ya ushambuliaji ya Chirwa a Ajibu, hawa wote wana akili nyingi, ninavyoona kama wataendelea kucheza pamoja watakuwa hatari zaidi.”

Yanga kesho Jumatano itashuka Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kupimana nguvu na Rhino ya Ligi Daraja la Kwanza.