Gymkhana yasherekea miaka 100 ya kuanzishwa kwake kwa mtindo wa kipekee

Muktasari:

Mwenyekiti wa DGC, Walter Chipeta alisema kusherehekea kutimiza miaka 100 kwa staili ya tofauti tangu kuanzishwa kwake mwaka 1916.

Dar es Salaam.  Klabu ya , Dar es Salaam Gymkhana Club (DGC) itasherekea kutimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake  kwa kufanyika mashindano ya michezo ya aina mbalimbali kuanza Julai 3 na kumalizikia Julai 8 .

Mwenyekiti wa DGC, Walter Chipeta alisema kusherehekea kutimiza miaka 100 kwa staili ya tofauti tangu kuanzishwa kwake mwaka 1916.

Miongoni michezo iliyopangwa kufanyika katika kuadhimisha miaka 100 ya klabu hayo ni pamoja na gofu, tenisi, skwashi, soka, kriketi, mchezo wa kuogelea na mingine mingi ambayo kwa ujumla itawahusisha wanachama na wasio wanachama wa klabu hiyo.

Mashindano hayo yamedhaminiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mwananchi Communication Ltd, Hotel ya Serena, Clouds media group, Qatar airways, GSM, na  Eco Africa.

Chipeta amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na klabu kadhaa zimethibitisha kushiriki katika mashindano hayo ambayo pia yataambatana na tafrija maalum ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kujenga chumba kwenye taasisi ya ugonjwa wa Saratani ya Ocean Road.

“Tunatarajia kuwa na michezo yenye kusisimua sana mashabiki, mbali ya soka ambayo itashirikisha timu mbalimbali, wachezaji wa gofu maarufu wa Afrika Mashariki nao watashiriki katika mashindano hayo ambapo washindi watazawadiwa zawadi mbalimbali,” alisema Chipeta.

Menaja Mauzo wa NHC, Itandula Gambalagi alisema kuwa wamemua kudhakini maadhimisho hayo kama sehemu ya kuchangia maendeleo ya michezo nchini kwani klabu ya Gymkhana ina michezo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo nchi.

“Hii ni faraja kwetu, kwa kushiriki katika maadhimisho haya, tutaweza kusaidia wachezaji wa tenisi, gofu, skwashi na kuogelea, tunaomba wadhamini wajitokeze ili kufanikisha miaka 100 ya klabu hii,” alisema  Gambalagi.