Gor Mahia uso kwa uso na Yanga

Saturday April 21 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Mabingwa mara 16 wa Ligi ya Kenya, Gor Mahia itaanzia kampeni yake ya Kombe la Shirikisho Afrika ugenini Rwanda kwa kuivaa Rayons Sports katika droo ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyofanyika muda mfupi uliopita, Jijini Cairo, Misri.

Baada ya mchezo huo wa ugenini, Gor Mahia watarudi nyumbani kuwakaribisha USM Alger kati ya Mei 15-16 na kupisha Kombe la Dunia.

Gor Mahia watawakarisha Yanga kati ya Julai 17-18. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Gor Mahia na Yanga kukutana tangu 1984.

Katika mchezo huo John Okello Zangi aliifungia Kogalo bao la kusawazisha katika sare ya 1-1 jijini Dar es salaam kabla Sammy Onyango Jogoo hajaiuwa Yanga kwenye mechi ya marudiano iliyopigwa jijini Nairobi na Gor ikashinda 1-0 na kufuzu kwa ushindi wa jumla wa 2-1.

Gor Mahia ilijikatia tiketi ya kutinga hatua hiyo baada ya kuifungisha virago Supersport United ya Afrika Kusini. Kogalo walisonga mbele kutokana na sheria ya goli la ugenini baada ya kuwafunga wapinzani wao 1-0 katika mechi ya kwanza, iliyochezwa Kenyatta Stadium Machakos, kabla ya kuchapwa 2-1 ugenini.

Yanga ilijikatia tiketi ya kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa goli 2-1 dhidi ya wapinzani wao Welayta Dicha ya ethiopia. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es salaam, Yanga ilishinda 2-0, kabla ya kukubali kichapo cha 1-0 ugenini.

Droo hiyo imehusisha jumla ya timu 16, kutoka mataifa 14 barani Afrika. Gor Mahia inayonolewa na Muingereza Dylan Kerr ipo katika Kundi D pamoja na Yanga (Tanzania), Rayon Sport (Rwanda na USM Algiers (Algeria).

Katika kundi A zipo Raja Casablanca, ASEc Mimosas, Aduana Stars na AS Vita Club, huku Kundi B ikiundwa na Al Masry, UD Songo, RS Berkane na Al Hilal Omdurman. Djoliba, Williamsville, AC CARA Brazaville na Enyimba FC zote zimepangwa katika kundi C.