Giroud kapenya

Muktasari:

  • Kwenye mechi hiyo, Kylian Mbappe alifunga bao la kwanza, Uholanzi ikasawazisha, lakini dakika za mwisho, OIivier Giroud akapiga bao la ushindi, linalomfanya kupenya kwenye Tano Bora ya Wafungaji Bora wa muda wote kwenye Timu ya Taifa ya Ufaransa.

UFARANSA imeichapa Uholanzi 2-1 kwenye Uefa Nations League juzi Jumapili. Hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza kucheza nyumbani tangu ilipotoka kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2018.

Kwenye mechi hiyo, Kylian Mbappe alifunga bao la kwanza, Uholanzi ikasawazisha, lakini dakika za mwisho, OIivier Giroud akapiga bao la ushindi, linalomfanya kupenya kwenye Tano Bora ya Wafungaji Bora wa muda wote kwenye Timu ya Taifa ya Ufaransa.

5.Zinedine Zidane- mabao 31, mechi 108

Zinedine Zidane alihitimisha maisha yake kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Ufaransa kwa maumivu baada ya kuchapwa kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2006. Zidane alifunga bao kwenye fainali hizo, lakini baadaye akatolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa beki wa Italia, Marco Materazzi. Alifunga mabao 31 katika mechi 108 alizoichezea Les Bleus.

4.Olivier Giroud- mabao 32, mechi 83

Straika Olivier Giroud amemaliza ukame wake wa mabao baada ya kufunga bao maridadi kabisa dhidi ya Uholanzi juzi Jumapili kwenye michuano ya Uefa Nations League.

Kiwango cha Giroud kwenye kufunga kilikuwa chini sana kwa siku za karibuni, lakini bao lake hilo limemfanya ampiku Zinedine Zidane kwenye orodha ya wafungaji bora kwenye kikosi cha Ufaransa. Straika huyo wa Chelsea sasa amefunga mabao 32 katika mechi 83 alizochezea Les Bleus.

3.David Trezeguet- mabao 34, mechi 71.

Gwiji wa Juventus, David Trezeguet hana muda mrefu atavukwa na Olivier Giroud kwenye chati za ufungaji bora kwenye Timu ya Taifa ya Ufaransa. Fowadi huyo wa zamani wa Ufaransa, alifunga mabao 34 katika mechi 71 alizoichezea timu hiyo. Kwenye kikosi cha Les Bleus alicheza sambamba na wakali Thierry Henry na Zinedine Zidane.

2. Michel Platini- mabao 41, mechi 72

Michel Platini ni mmoja kati ya wachezaji wenye rekodi zao tamu kwenye kikosi cha Ufaransa. Kiungo huyo mshambuliaji aliichezea Ufaransa mechi 72 na kufunga mabao 41.

Alikuwa akishikilia rekodi ya kuwa kinara wa mabao kabla ya Thierry Henry kuja kumpiku. Platini, aliyewahi kuichezea Juventus, ameshinda pia Tuzo ya Ballon d’Or mara tatu.

1.Thierry Henry- mabao 51, mechi 123

Kofia ya kinara wa muda wote wa mabao kwenye kikosi cha Ufaransa kwa sasa inavaliwa na Thierry Henry. Straika huyo kiwembe alifunga mabao 51 katika mechi 123 alizoitumikia Les Bleus. Ndiye mchezaji namba mbili aliyecheza mechi nyingi zaidi kwenye kikosi cha Ufaransa nyuma ya Lilian Thuram, aliyecheza mechi 142.

Henry yeye hadi anatundika daruga, amecheza mechi 123 kwenye kikosi cha Ufaransa.