Domingos aongeza mzuka mpya Msimbazi

Muktasari:

  • Kusajiliwa kwa straika huyo kutoka Msumbiji aliyepewa mkataba wa miaka miwili kama ilivyokuwa kwa beki wa kati kutoka Ghana, Asante Kwasi aliyekuwa akiichezea Lipuli FC, kumeongeza mzuka kwa mashabiki wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara.

MZUKA umepanda Msimbazi, baada ya Simba kukamilisha usajili wa dirisha dogo kwa kuwanasa nyota wawili wa kigeni akiwamo straika Dayo Antonio Domingos kutoka Msumbiji.

Kusajiliwa kwa straika huyo kutoka Msumbiji aliyepewa mkataba wa miaka miwili kama ilivyokuwa kwa beki wa kati kutoka Ghana, Asante Kwasi aliyekuwa akiichezea Lipuli FC, kumeongeza mzuka kwa mashabiki wa vinara hao wa Ligi Kuu Bara.

Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma alifichua kuwa, kutua kwa Domingos aliyekuwa Ferroviario de Beira, kutalifanya benchi la ufundi kubadilisha mfumo wao wa uchezaji mbele.

Djuma aliyetua Simba akitokea Burundi, alisema kuanzia sasa wataanza kutumia mfumo mpya wa kuchezesha mastraika wawili ili Simba itishe zaidi.

Aliyasema hayo baada ya straika wake John Bocco kufunga mabao manne katika mechi mbili za kirafiki dhidi ya KMC na African Lyon.

“Ninavyoiangalia timu yetu ilivyo kwa sasa na kwa usajili ambao, tumeufanya katika eneo la ushambuliaji nadhani tukiwatumia mastraika wawili ili tufunge mabao mengi zaidi ya mzunguko wa kwanza,” alisema na kuongeza: “Tunao mastraika wa kati watatu Juma Liuzio, Domingos aliyeingia kikosini na Bocco, wakicheza kwa pamoja wataongeza kasi ya ufungaji kwani, tunataka ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kutetea Kombe la FA na kufanya vema Kombe la Shirikisho Afrika,” alisema Djuma.

Kocha huyo aliyeiongoza Simba kucheza mechi mbili za kirafiki na kuvuna mabao saba, huku timu yake ikifungwa bao moja, alisema atakaa na bosi wake, Joseph Omog kujipanga upya.

“Nitamshauri Kocha Mkuu (Joseph Omog) juu ya hili na nina aimani kubwa ataelewa na tutaanza kucheza hivyo katika mechi zijazo,” aliongezea Djuma.