David Silva atundika daluga Hispania

Manchester, England. Kiungo wa Manchester City, David Silva, ametangaza kustaafu kuitumikia timu ya Taifa ya Hispania, baada ya kuitumikia mfululizo kwa miaka 12.

Silva alianza kuitumikia Hispania kuanzia mwaka 2006 hadi alipotangaza kustaafu juzi, alikuwa ameichezea jumla ya mechi 125 na kufunga mabao 35, akitwaa mataji mawili ya ubingwa wa Ulaya mwaka 2008 na 2012 na taji ubingwa wa Dunia mwaka 2010.

Mchezaji huyu wa zamani wa Valencia, mwenye miaka 32 alisema kwa sasa umri wake umekwenda hivyo anaona bora kuelekeza nguvu zake kwenye timu ya Manchester City na kuwachia vijana majukumu kwenye timu ya Taifa.

Alisema anajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya timu ya Taifa ya Hispania na siku zote atajivunia kwa hilo. “Ni jambo kubwa sana nitakuwa na kumbukumbu nzuri kwenye medani ya soka yapo mambo nitakayoyakumbuka daima,” alisema.

Alisema kuwa licha ya kuwa na wazo hilo kwa kipindi kirefu lakini alichukua muda mrefu kufikia maamuzi kutokana na ukweli kwamba ni jambo linalougusa moyo wake na mioyo ya wengi.

Kustaafu kwa mchezaji huyo kumekuwa ni muendelezo wa wachezaji wa Hispania kustaafu, wiki iliyopita mlinzi mahiri wa Barcelona, Gerard Pique alitangaza kustaafu kuitumikia timu ya Taifa akiwa na miaka 31.