#WC2018: Cheki wababe wa Kombe la Dunia

Muktasari:

Mwaka huu kila nchi inataka ubingwa ili kutanua historia yake.

London,England

 

Maisha yanakwenda kasi sana, zimebaki siku chache tu kabla ya kupigwa kwa mtanange wa Kombe la Dunia kule Russia 2018. 

Mwaka huu kila nchi inataka ubingwa ili kutanua historia yake.

Lakini, katika fainali hizo kuna timu 32 zitawania nafasi ya kutwaa taji hilo, ambalo ni  timu nane tu ambazo zimewahi kufanikiwa kulitwaa.

 

Brazil (Mara tano)

Brazil ndiyo inayoongoza kuwa timu yenye mafanikio katika Fainali za Kombe la Dunia, baada ya kutwaa taji hilo mara tano. Brazil ilitwaa taji hilo nchini Sweden 1958, Chile 1962, Mexico 1970, Marekani 1994 na Korea/Japan 2002. Brazil ilitwaa taji hilo katika mabara manne ambayo ni Ulaya, Amerika ya Kusini, Amerika ya Kaskazini na Asia. Brazil ilishika nafasi ya pili mara mbili, 1950 na 1998 baada ya kufungwa na Uruguay na Ufaransa. Brazil pia ndiyo nchi ambayo imeshiriki katika fainali zote za Kombe la Dunia tangu mwaka 1930 mpaka 2014

 

Italia (Mara nne)

Italia imetwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mara nne. Italia ilitwaa taji hilo nchini Italia 1934, Ufaransa 1938, Hispania 1982 na Ujerumani 2006. Pia, Italia imeshika nafasi ya pili mara mbili (1970 na 1994) huku ikishika nafasi ya tatu mwaka 1990 na nafasi ya nne mwaka 1978. Imeshiriki mara 18.

 

Ujerumani (Mara nne)

Kati ya 1950 na 1990, timu iliyokuwa ikiitwa Ujerumani Magharibi ilitwaa ubingwa wa dunia mara tatu. Ujerumani Magharibi ilitwaa ubingwa kule Uswisi 1954, Ujerumani 1974 na Italia 1990. Ujerumani imemaliza katika nafasi ya pili mara nne ambazo ni 1966 nchini England, 1982 nchini Hispania, 1986 nchini Mexico na 2002 huko Korea/Japan. Kati ya 1930 mpaka 2014 Ujerumani imeshiriki Fainali za Kombe la Dunia mara 18. Mwaka 2014, Ujerumani ilitwaa ubingwa wa dunia kwa mara ya nne.

 

Argentina (Mara mbili)

Mwaka 1978, Argentina ilikuwa ni taifa la tano kutwaa ubingwa wa dunia. Ilitwaa tena ubingwa wa dunia mwaka 1986. Argentina imeshika nafasi ya pili katika fainali za dunia mara tatu, mara ya kwanza ilikuwa 1930 nchini Uruguay, mara ya pili 1990 kule Italia na mara ya tatu mwaka 2014 ndani ya ardhi ya Brazil. Tangu 1930 mpaka 2014, Argentina imeshiriki Fainali za Kombe la Dunia mara 16.

 

Uruguay (Mara mbili)

Uruguay iliandaa na kutwaa ubingwa wa dunia katika fainali za kwanza zilizofanyika 1930, pia ilitwaa ubingwa wa dunia kwa mara ya pili mwaka 1950 nchini Brazil. Tangu 1930 mpaka 2014, Uruguay imeshiriki Fainali za Kombe la Dunia mara 14.

 

  Ufaransa (Mara moja)

Ufaransa imetwaa ubingwa wa dunia mara moja mwaka 1998 walipoandaa fainali hizo. Walifika fainali mwaka 2006, lakini walifungwa na Italia.  Ufaransa imeshiriki mara 14.

 

Hispania (Mara moja)

Hispania imetwaa ubingwa wa dunia 2010 nchini Afrika Kusini. Ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa Uholanzi 1-0. Pia, iliwahi kushika nafasi ya nne mwaka 1950 na imefika hatua ya robo fainali mara nne. Tangu mwaka 1930 mpaka 2014, Hispania imeshiriki  mara 14.

 

England (mara moja)

England iliandaa na kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 1966 baada ya kuichapa Ujerumani 4-2 na haijawahi kubeba tangu wakati huo.

Pia, England imewahi kushika nafasi ya nne, vilevile imewahi kufika hatua ya robo fainali mara sita.