Chama, Dilunga wamtesa Mbelgiji

Muktasari:

Katika msimu uliopita, Kocha Pierre Lechantre hakuwa anawatumia sana viungo ndio maana maana alikuwa akiwapiga benchi Mzamiru Yassin, Mohammed Ibrahim, Haruna Niyonzima, Said Ndemla na Mwinyi Kazimoto ambaye alitimkia JKT Tanzania.

MNAKUMBUKA ule msala uliwahi kumpata Kocha Joseph Omog juu ya viungo wake, Jonas Mkude na James Kotei? Kama mmesahau Omog alikuwa akimpanga Kotei na kumweka benchi Mkude, jambo lililomfanya acharukiwe na mashabiki, kabla ya baadaye kuamua kuwatumia wote pamoja kwa nafasi tofauti.

Sasa msala kama huo unataka kumtokea Kocha Patrick Aussems ambaye jioni ya jana alikuwa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara kuiongoza timu yake dhidi ya

Ndanda akiwa na mtihani wa kumtumia kati ya Hassan Dilunga na Cletus Chama.

Katika msimu uliopita, Kocha Pierre Lechantre hakuwa anawatumia sana viungo ndio maana maana alikuwa akiwapiga benchi Mzamiru Yassin, Mohammed Ibrahim, Haruna Niyonzima, Said Ndemla na Mwinyi Kazimoto ambaye alitimkia JKT Tanzania.

Lakini Kocha wa sasa, Aussems amesisitiza kuwa kikosi chake lazima kiwe na viungo watatu, huku kikosi kwake kuwa na vichwa matata wanamchanganya.

Aussems aliliambia Mwanaspoti; “Kila kocha huwa na uamuzi wake na hufanya kile ambacho anaamini kitampa matokeo mazuri, hivyo hata kwangu kwani viungo wote niliowakuta hapa ni wazuri ndio maana nimewatumia wote katika mechi mbalimbali ili kutambua na kuona uwezo wa kila mmoja.

“Cletus Chama, Hassan Dilunga, Ibrahim, Ndemla na Mzamiru ni viungo washambuliaji bora ambao wapo katika kikosi changu na nina uwanja mpana wa kuchagua kumtumia yoyote yule kulingana na mechi husika.

“Lakini kumekuwa na michuano mkubwa kati ya Chama, Dilunga na Ibrahim ambao hawa katika timu yangu mbali ya kuwa kiungo wa kati nitakuwa

nawatumia pembeni pia, “ alisema.

“Navutiwa na ushindani wao wanaonyesha kweli kila mmoja anastahili kupata nafasi ya kucheza na hata mechi mbili za ligi nilimtumia Dilunga alicheza vizuri lakini alitoka na nafasi yake alicheza Mzamiru mechi zote mbili ya Prisons na ile ya Mbeya City alitoka akaingia Ndemla, nao walicheza vizuri pia, “ alisema.

Chama hakucheza mechi yoyote ya kimashindano kwani (ITC) yake ilichelewa kufika lakini alicheza mechi za kirafiki kabla ya msimu kuanza na kuonesha soka la

kiwango cha juu jambo lililofanya kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba.

Tangu kuja kwa kocha Aussems kiungo Ibrahim amekuwa akipata nafasi ya kuaminiwa na kocha huyo na huenda akaonyesha ubora wake zaidi mechi zijazo.

Chini ya Lechantre, Ibrahim alikuwa mchezaji wa kukaa benchi kwa madai ya kushindwa kuonesha nidhamu nzuri mbele ya kocha huyo ambaye kwa sasa anafundisha soka Libya.

ETI OKWI ANA MADENI MATATU

MFUNGAJI Bora wa msimu uliopita, Emmanuel Okwi amefunguka akidai ana madeni matatu ya kulipa msimu huu.

Msimu uliopita Okwi alimaliza Ligi na mabao 20 lazima kwa sasa ameweka wazi kuwa anahitaji kufunga mabao 30, kutetea ubingwa wa Ligi na kuchukua Kombe la FA.

Pia alisema atafurahi zaidi kuona Simba ikimaliza msimu ikiwa na mabao mengi kuliko ya msimu uliopita ambapo walifunga mabao 62 kwa utatu mtakatifu wake, John Bocco na Shiza Kichuya.

“Nilifunga 20 katika ligi nataka kufunga zaidi ya hayo licha ya kukosa mechi mbili lakini nina uwezo na najiamini kufanga zaidi. Katika mechi za Kombe la Shirikisho nilifunga mabao matatu, msimu huu nataka kufunga zaidi ya hayo na nataka nifunge katika Ligi mabao yasiyopungua 30,” alisema Okwi.

“Kama nikiweza kufanya hivyo nitakuwa nimeisaidia timu yangu kwa kiasi kikubwa kabla ya kujiangalia mimi nimefanya nini zaidi,” alisema Okwi.

Okwi alikwenda mbali zaidi na kufunguka jambo la pili katika ligi msimu uliopita walimaliza wakiwa mabingwa, kwa jinsi kikosi chao kilivyo wana kila sababu ya kutetea ubingwa huo.

“Tumefanya maandalizi ya kutosha nchini Uturuki, usajili mzuri umefanyika ndani ya timu na kila kitu muhimu kwa wachezaji kinapatikana kwa wakati na hilo limechangia kikosi chetu kuwa na morali ya hali ya juu.

“Vile vile kama Simba tumejipanga kuhakikisha tunavuka hatua ambayo tuliishia msimu uliopita kwenye michuano ya Kimataifa ambayo msimu huu tutaiwakilisha Tanzania katika Klabu bingwa Afrika,” alisema.