Cannavaro alisajiliwa kwa supu na mikate tu

HABARI mbaya kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ni kukaribia kuanza bila kujulikana kwa mdhamini mkuu, lakini pale Yanga ndio kuna habari mbaya zaidi.

Yanga itaanza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara bila ya nahodha wake wa mfano kabisa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, ambaye ametundika daruga zake rasmi.

Jina Cannavaro halitakuwepo msimu ujao na kama litakuwepo basi halitakuwa uwanjani bali kwenye karatasi tu. Msimu ujao beki huyo kitasa atakuwa akionekana ameshika karatasi kwenda kwa mwamuzi wa akiba kwa ajili ya kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake.

Cannavaro amestaafu rasmi kucheza soka la ushindani na wiki iliyopita aliagwa kwa mara ya kwanza pale Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na sasa anaanza majukumu yake mapya kama Meneja wa Yanga.

Kustaafu kwa Cannavaro hakuwezi kuwa habari nyepesi na kupita kirahisi tu bila mashabiki wa soka kumfahamu kwa undani na kama kawaida Mwanaspoti, likafanya naye mahojiano maalumu.

Lakini, pamoja na mambo mengine Mwanaspoti likataka kufahamu chimbuko la jina la Cannavaro na aliyempachika jina hilo ambalo limedumu kwa miaka mingi kwelikweli.

“Cannavaro asili yake lilitokea Zanzibar na nilipewa na kocha wangu, Hassan Haji Hamza Chura, ambaye ni kocha aliyenifundisha nikiwa mdogo,” anaanza kwa kusimulia Cannavaro.

“Ni jina ambalo hata mitaani linajulikana kuliko Nadir Haroub, ukifika hata pale bandarini Zanzibar ukawaambia nataka kwenda nyumbani kwa kina Cannavaro utapelekwa moja kwa moja. Nilipewa wakati ule beki wa Italia, Fabio Cannavaro alipokuwa anawika akiwa na kina Alexandro Nesta.

Alikoanzia hadi kutua Yanga

“Nimeanza kucheza soka Zanzibar katika timu ya Kuwait, unajua kule kuna ligi mpaka za vijana baada ya hapo nilihamia timu ya Medisani na nilidumu hapo hadi nilipoanza kuchezea timu za Ligi Kuu.

“Baada ya kucheza hapo kwa muda ndipo Yanga wakaniona na kuvutiwa na kiwango changu. Yanga waliniona katika mashindano ya Chalenji kuna meneja wangu alikuwa anaitwa Ally Dai, ambao walimwona na kufanya naye mazungumzo. Alifanya mazungumzo na bosi wa Yanga wakati huo, Francis Kifukwe na tukakubaliana na hapo tukaingia dili,” anasema.

Usajili wake wa kwanza

(Anacheka kidogo) “Usajili wangu wa kwanza kabisa watu wanaweza kucheka na wasiamini, lakini kwangu ni historia ambayo kamwe siwezi kuisahau. Kwanza mara ya kwanza kabisa nilisajiliwa baada ya kupewa supu, mikate miwili na jozi ya viatu vya soka.

“Wakati huo nikitokea Kuwait kwenda Medisani sikupewa hata senti moja na aliyefanikisha usajili huo ni Kocha Chura, nilikubali kuchukua vitu hivyo kwa kuwa kiu yangu haikuwa fedha bali nilihitaji zaidi kucheza mpira. Labda kwenye vitu hivyo kikubwa ambacho nilikiona cha thamani kubwa kwangu ni vile viatu.”

Yanga alichukua sh ngapi

Wakati Cannavaro anatua Yanga mwaka 2005 kila mtu alimwona ni mchezaji wa kawaida kwa kuwa, hawakupata nafasi ya kuona makali yake kama ilivyokuwa kwa Kifukwe.

Cannavaro alipiga mpira mwingi kwenye michuano ya Chalenji akiwa na timu ya Taifa ya Zanzibar iliyofanyika kule Rwanda.

Hata hivyo, mara baada ya kutua na kuanza kuonyesha shughuli yake uwanjani, kuna baadhi ya mashabiki na viongozi wa Yanga hawafahamu siri nzito iliyojificha ndani yake na hapa Cannavaro anafichua ishu nzima.

“Kwangu kucheza soka ndio kila kitu na Yanga waliniahidi kunipa nafasi ya kucheza, katika usajili wangu walinipa Sh1 milioni kama pesa ya usajili na mshahara wangu wa kwanza ulikuwa Sh100,000 kwa mwezi.

“Hivyo ndivyo nilivyoanza maisha yangu ya soka na mpaka sasa naondoka pengine niweke wazi kuwa, dau kubwa ambalo nimewahi kuchukua ni Sh60 milioni hadi natangaza kustaafu soka nikiwa Yanga.

Maisha yake ndani ya Yanga

“Kwanza niseme tu nilikuwa mmoja wa wachezaji wenye bahati kubwa ndani ya Yanga, nilikuwa naishi maisha mazuri sio mashabiki sio viongozi mpaka wachezaji wenyewe kila mmoja alikuwa akinipenda.

Kila nilichokuwa nahitaji nilikuwa natimiziwa na kama hakipatikani kwa wakati huo basi navumilia.

Hiyo ndio sababu kubwa ikitokea mtu akaniuliza ni nani alinisaidia katika maisha yangu ndani na nje ya uwanja, basi jibu ni Yanga.

Siri ya kudumu Yanga

Cannavaro ni miongoni mwa wanasoka wachache waliocheza soka la ushindani na kwa kiwango cha juu kwa muda mrefu bila kuchuja.

Tangu ametua Yanga hadi anatangaza kustaafu soka la ushindani na kupewa wadhifa mpya wa Meneja wa Timu, Cannavaro amedumu Jangwani kwa miaka 13.

Ndani ya miaka hiyo amekuwa kiongozi wa wachezaji na mchezaji muhimu panga pangua hakosi namba kwenye kikosi cha kwanza, labda awe majeruhi ama mgonjwa ndio anaweza kukosekana.

Hata hivyo, anafichua siri pekee iliyomfanya kudumu kwa muda mrefu ndania timu moja huku akilinda kiwango chake.

“Nidhamu nje na ndani ya uwanja ni vitu muhimu sana kwa mchezaji na hivyo, vimenifanya nidumu Jangwani kwa muda mrefu huku nikilinda pia kipaji changu. Kujali wakubwa na wadogo na kuweka usawa ndio vitu ninavyovipenda.

Nahodha wa ukweli

Unamkumbuka Roy Keane au Patrick Viera? Kama umewasahau basi hawa jamaa walikuwa manahodha wa ukweli kwenye klabu zao za Man United na Arsenal.

Jamaa hawakuwa legelege hata kidogo na walikuwa wababe ndani na nje ya uwanja, lakini walikuwa wakarimu sana na wanapiga mpira mwingi kwelikweli.

Kwa Cannavaro unaweza kuwaona tena aina ya manahodha hawa wawili walioishika Ligi Kuu ya England. Mkongwe huyu anaweza kuwa na rekodi za aina yake kwani, mpaka anastaafu ndiye mchezaji aliyezitumikia timu za taifa mbili na zote amewahi kuwa nahodha kwa wakati mmoja, pia Yanga alikuwa nahodha.

“Kweli nimetumikia kwa muda mrefu timu za taifa na hili lilitokana na mapenzi yangu ya dhati kwa taifa langu, hata viongozi wa TFF waliopita kuanzia Leodgar Tenga na Jamal Malinzi walikuwa wakinikubali, lakini ilifika muda ilibidi niachane na majukumu hayo.

Tukio hili hatalisahau

Kila mchezaji anaona fahari kuitumikia timu ya taifa lake na kwa Cannavaro hilo halina utata kabisa kwani, hadi anapewa unahodha tayari uwezo wake unajulikana.

Hata hivyo, beki huyo aliachana na soka la kimataifa kwa staili tofauti huku ikielezwa kuwa, hakuvutiwa na maamuzi ya kocha mkuu wakati huo akiwa Charles Mkwassa, ambaye aliteua nahodha mpya kuchukua nafasi ya Cannavaro bila kumshirikisha.

“Ni kweli niliachana na soka la kimataifa kwa namna tofauti kidogo na hilo ni kutokana na tukio la kocha kutangaza kubadilisha nahodha mpya bila kunishirikisha. Ki ukweli sikuona kama nimepewa heshima hivyo, nikaona ni vyema niachane na majukumu hayo.

“Shida haikuwa kuteuliwa kwa nahodha mpya, tatizo lilikuwa ni mawasiliano na heshima yangu na hapo hapo nilitafakari na kutangaza kuachana na soka la kimataifa.”

Mechi alizocheza Stars

“Siwezi kukumbuka mechi nilizochezea timu ya taifa, lakini ni nyingi ila ninachokumbuka ni idadi ya mabao niliyoyafunga timu za taifa ni matano tu.

Penalti za Panenka

Cannavaro alikuwa akiwarusha roho makocha, wachezaji, viongozi na hata mashabiki kwa staili yake ya upigaji wa penalti maarufu kama Panenka, ambazo mpigaji anajiandaa akitokea mbali kama anapiga shuti kisha anauchimbua mpira kwa kiatu chake kwa ufundi mkubwa.

“Aaah inataka moyo sana kupiga vile hasa kwenye mechi kubwa, unajua nimepiga panenka mbili, moja nilifunga na nyingine nilikosa.

“Penalti niliyokosa ilikuwa dhidi ya Gor Mahia ya Kenya miaka ya nyuma kidogo ambayo tulipoteza kwa 2-1 na kama ningepata ilikuwa naisawazishia Yanga, sikutumia nguvu nilipiga kipa akadaka na zilikuwa ni dakika za mwisho kabisa.

“Penalti nyingine ilikuwa dhidi ya Al Ahly kule kwao mechi ambayo mshindi aliamuliwa kwa penalti, nilirudia staili ile ile ya upigaji na nikafunga, lakini niliendelea kujiamini ndiyo maana nilikuwa nafanikiwa.

Kocha alimwambia nini?

Wakati Cannavaro anapiga panenka na kufunga dhidi ya Al Ahly, kocha Mholanzi Hans Pluijm alimfuata na kumweleza jambo na hapa anafunguka: “Kocha aliniita baada ya kupiga vile akanikataza akaniambia nisifanye tena kitu kama kile kwani, naweza kumuua kwa presha. Nakumbuka hata Jerry Tegete alinifuata na kuniambia: ‘wewe jamaa ni chizi sana’.

Unafahamu Cannavaro alikaribia kuacha soka kisa Simba na unajua alibakiza dakika chache tu kusaini kuichezea Simba? Hakikisha unafuatilia simulizi hii kesho Ijumaa.