Caf yairejesha upya Ligi ya Muungano

Muktasari:

Kitendo cha Zanzibar kupokonywa uanachama, kimevifanya visiwa hivyo kupoteza nafasi ya klabu zake kushiriki wa Ligi ya Mabingwa na Kombe a Shirikisho Afrika mbali na timu zake za taifa kuzuiwa kushiriki 

HAKUNA namna zaidi ua kurejeshwa kwa Ligi ya Muungano katika soka la  nchini ikiwa ndio njia  sahihi ya kumaliza sintofahamu iliyojitokeza kutokana na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) kuivua uanachama Zanzibar.

Kamati ya Utendaji ya Caf iliyoketi wiki iliyopita jijini Rabat, Morocco iliipokonya Zanzibar uanachama wake kwa vile Katiba ya shirikisho hilo hairuhusu kuvipatia uanachama vyama viwili vya soka ambavyo viko ndani ya nchi moja.

Kitendo cha Zanzibar kupokonywa uanachama, kimevifanya visiwa hivyo kupoteza nafasi ya klabu zake kushiriki wa Ligi ya Mabingwa na Kombe a Shirikisho Afrika mbali na timu zake za taifa kuzuiwa kushiriki mashindano yote  yanayoandaliwa na Caf pamoja na shirikisho la vyama vya soka duniani (FIFA).

Awali klabu za Zanzibar zilishiriki mashindano ya klabu Afrika licha ya visiwa hivyo kutokuwa mwanachama wa Caf, hivi sasa fursa hiyo haitokuwepo tena kutokana na kupoteza nafasi hiyo Ijumaa iliyopita.

“Mwanzoni klabu za visiwani zilikuwa zikipata nafasi ya kushiriki mashindano ya klabu Afrika kwa sababu Zanzibar ilipewa ‘provisional membership’ (uanachama wa muda) na Caf hivyo klabu zake zikawa zinashiriki huku ikisubiri kupatiwa uanachama wa kudumu,” alisema Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Angetile Osiah.

“Kwa bahati mbaya Caf imewapokonya uanachama ambao walishafanikiwa kuupata, hivyo klabu zake hazitoweza kushiriki tena kwenye mashindano ya klabu kwa tiketi ya kuiwakilisha Zanzibar na kwa mtazamo wangu, kwa sasa kinachotakiwa ni kurudisha tu Ligi ya Muungano.”

Mtazamo huo wa Osiah uliungwa mkono na Katibu Mkuu wa zamani wa ZFA, Mohammed Ally, ambaye licha ya kutaja Ligi ya Muungano kama suluhisho la muda mfupi, alitoa wito wa kupatikana dawa ya muda mrefu kumaliza sintofahamu iliyogubika wadau wa soka baada ya Zanzibar kupokonywa uanachama.

“Sisi upande wa Zanzibar hili suala hatujalipokea vizuri na tumeliona kwamba limeturudisha miaka 100 nyuma kwani tumefanya harakati za kuhakikisha tunapewa uanachama wa Caf na FIFA,” alisema Ally.

“Ninachoshauri kwanza ni serikali zote mbili kufanya mapitio  ya sehemu zinazohusu michezo katika Muungano wetu na ikiwezekana ikutanishe vyama vya soka vya Bara na Zanzibar na kuangalia namna ya kulisaidia soka la Zanzibar.

“Ila kuna haja ya kuirudisha Ligi ya Muungano ili iweze kusaidia kupatikana kwa wachezaji wazuri wa kuunda timu ya taifa pamoja na kupata klabu wawakilishi wa nchi kwenye mashindano ya kimataifa.”

Ligi ya Muungano ilizimika rasmi mwaka 2004 baada ya Zanzibar kutambuliwa na Caf na ikawa inatoa wawakilishi wake moja kwa moja katika michuano ya Afrika.