Biashara Utd, Kagera Sugar kukata utepe

Muktasari:

Timu hizo zinatakuta kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Karume, Musoma katika mechi ya Ligi Kuu

Dar es Salaam. Kocha wa Biashara United, Hitimana Thierry amesema wanataka kuuzindua uwanja wao wa Karume Musoma kwa ushindi dhidi ya Kagera Sugar leo Jumamosi jioni.

Biashara itashuka kwenye Uwanja huo leo kwa mara ya kwanza kuikabili Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu bara utakaoanza sasa 10:00 jioni.

Uwanja huo ulikuwa katika ukarabati kwa muda mrefu na sasa tayari umekamilika na kuruhusiwa kuanza kutumika.

Hitimana alisema wamejiandaa vizuri na mchezo huo na matarajio yao ni kushinda ili kuwapa raha mashabiki wao.

"Naamini mashabiki wetu walikuwa na hamu ya kutuona hivyo waje kwa wingi kutusapoti kama ilivyokuwa mwanzo na sisi hatutawaangusha.

"Natarajia mchezo mgumu kwani Kagera Sugar sio timu ya kubeza.Tutapambana ili kupata matokeo mazuri kwani tunataka kuanza kutumia uwanja na ushindi"alisema Hitimana.

Naye kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema wamejiandaa vizuri na mchezo huo na anaimani watapata wakati mgumu kwani wako ugenini, lakini watakomaa ili kupata ushindi.